WAFUGA MBWA DODOMA WAIOMBA SERIKALI KUPUNGUZA KODI YA CHANJO NA MADAWA


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Umoja wa Wafuga Mbwa Mkoa wa Dodoma umeiomba Serikali kuweka mazingira rafiki kwa sekta ya ufugaji wa mbwa kwa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa chanjo na kupunguza kodi ya madawa pamoja na vyakula vya mbwa, hatua ambayo itaongeza hamasa kwa wafugaji na kuboresha ubora wa mifugo hiyo.


Ombi hilo limetolewa leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Umoja wa Wafuga Mbwa Mkoa wa Dodoma, Nganile Mwakasege, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la umoja huo kwenye Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane.


Mwakasege amesema gharama za chanjo, madawa na vyakula vya mbwa bado ni kubwa, jambo linalowakatisha tamaa baadhi ya wafugaji na kuathiri maendeleo ya sekta hiyo.


"Tunaiomba Serikali itoe kipaumbele katika upatikanaji wa chanjo na pia ipunguze kodi kwenye madawa na vyakula vya mbwa ili wafugaji wapate hamasa ya kufuga mbwa bora wenye viwango vinavyokubalika," amesema.


Aidha, amesema ushiriki wa umoja huo katika Maonesho ya Nane Nane unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika ufugaji wa mbwa pamoja na kuonesha aina mbalimbali za mbwa wanaofugwa nchini.


Amefafanua kuwa katika banda lao, wananchi wanapata nafasi ya kujionea mbwa wa ulinzi, mbwa wa urembo na kujifunza mbinu bora za ufugaji, lishe, afya pamoja na namna ya kuwalea kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya kisasa.


Mwakasege ametoa wito kwa Watanzania kutembelea banda hilo lililopo karibu na Kijiji cha Protein katika viwanja vya Maonesho ya Nane Nane ili kupata elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu ufugaji wa mbwa.


Amesema baada ya maonesho hayo kumalizika, huduma za ushauri na mafunzo zitaendelea kutolewa katika ofisi za Umoja wa Wafuga Mbwa Mkoa wa Dodoma zilizopo karibu na Hospitali ya Milembe, ambapo wafugaji na wananchi wataweza kupata msaada wa kitaalamu kuhusu sekta hiyo.

Previous Post Next Post