TFC YAAGIZA TANI 200,000 ZA MBOLEA, YAWEKEZA VIWANDA KUONGEZA TIJA YA KILIMO.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kuongeza upatikanaji wa mbolea nchini kwa kuagiza tani 200,000 za mbolea kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2026/2027, sambamba na uwekezaji katika viwanda vya kuchanganya mbolea na uchakataji wa chokaa ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.


Akizungumza Agosti 1, 2026, katika Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samuel Ahadi Mshote, alisema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora kwa wakati, kwa bei nafuu na inayokidhi mahitaji ya mazao pamoja na afya ya udongo.


Alisema katika awamu ya kwanza TFC imeagiza tani 70,000 za mbolea, ambapo tani 35,000 za mbolea aina ya DAP tayari zimewasili nchini na zinafungashwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima kupitia mpango wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali.


Aidha, alisema tani nyingine 40,000 za mbolea aina ya Urea zinatarajiwa kuwasili nchini ndani ya muda mfupi ili kuhakikisha mahitaji ya msimu wa kilimo yanakidhiwa kikamilifu.


"Tunataka kuhakikisha hakuna mkulima anayekosa mbolea kutokana na changamoto za upatikanaji. Ndiyo maana tumeongeza kiwango cha uagizaji na kuimarisha mtandao wa usambazaji nchini kote," alisema Mshote.


Alieleza kuwa TFC imepanua mtandao wake wa huduma kwa kuongeza vituo vya mauzo kutoka nane hadi 26 vinavyohudumia mikoa 22 ya Tanzania Bara, hatua ambayo imewafanya wakulima kupata huduma karibu na maeneo yao.


Mbali na vituo hivyo, alisema kampuni hiyo inashirikiana na zaidi ya mawakala 600 wa pembejeo za kilimo, Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) 29 pamoja na halmashauri mbalimbali ili kuhakikisha mbolea zinawafikia wakulima hadi ngazi ya vijiji.



Mshote alisema tangu TFC ilipoanza kusambaza mbolea mwaka 2022, zaidi ya tani 350,000 za mbolea za ruzuku zimesambazwa kwa wakulima wanaozalisha mpunga, mahindi, mboga mboga, vitunguu pamoja na mazao mengine ya biashara.


Katika hatua nyingine, alisema kampuni hiyo inakamilisha ufungaji wa mtambo wa kisasa wa kuchanganya mbolea jijini Dar es Salaam wenye uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za mbolea kwa mwaka kulingana na mahitaji ya udongo na mazao mbalimbali.



Alisema uwekezaji huo utapunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa mbolea maalumu kwa mazao ya kimkakati yakiwemo vitunguu, ufuta, parachichi na mazao mengine yenye thamani kubwa kiuchumi.


Sambamba na hilo, Mshote alisema TFC imeanza kutekeleza mradi wa uchimbaji na uchakataji wa chokaa mkoani Tanga baada ya kupatiwa eneo na Halmashauri ya Jiji la Tanga. 


Alisema chokaa hicho kitasaidia kurekebisha tindikali kwenye udongo na pia kitakuwa malighafi muhimu katika uzalishaji wa mbolea.


Kwa mujibu wa Mshote, mafanikio ya mpango wa ruzuku ya mbolea yameongeza matumizi ya mbolea nchini kutoka tani 300,000 hadi zaidi ya tani milioni 1.2 kwa mwaka, huku asilimia 80 ya wanufaika wakiwa wakulima wadogo.


Alisema ongezeko hilo limechangia kuimarika kwa uzalishaji wa mazao na kuiwezesha Tanzania kufikia zaidi ya asilimia 130 ya kujitosheleza kwa chakula.


Aidha, matumizi ya mbolea kwa hekta yameongezeka kutoka kilo 16 hadi kilo 24, huku Serikali na wadau wa sekta ya kilimo wakilenga kufikia matumizi ya kilo 30 kwa hekta kwa mujibu wa Azimio la Abuja kuhusu matumizi ya mbolea barani Afrika.


Mshote alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za umma na wananchi ili kuhakikisha malengo ya kuongeza tija, ushindani na ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya kilimo yanafikiwa.


Aliwataka wakulima kutembelea banda la TFC katika Maonesho ya Nane Nane ili kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, aina zinazofaa kwa mazao yao pamoja na teknolojia mpya zinazolenga kuongeza uzalishaji na kipato cha mkulima.

Previous Post Next Post