Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kushiriki Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, ukiwahimiza wafanyabiashara, wakulima na wajasiriamali kurasimisha shughuli zao za kiuchumi ili kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo.
Huduma hizo zinatolewa kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026, ambapo wananchi wanapata huduma zote muhimu zinazotolewa na BRELA bila kulazimika kufika katika ofisi za taasisi hiyo.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafyuka, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa kusajili biashara zao ili ziweze kukua, kupata uaminifu na kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema huduma zinazotolewa ni pamoja na usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A, usajili wa alama za biashara na viwanda, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu huduma zote zinazotolewa na BRELA.
"Tunawakaribisha wafanyabiashara, wakulima na wananchi wote kutembelea banda letu. Mbali na kupata huduma mbalimbali, watapata elimu itakayowawezesha kurasimisha biashara zao na kuzikuza kwa manufaa yao na uchumi wa taifa," amesema Mwasakafyuka.
Aidha, amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa BRELA kutambulisha mfumo mpya wa usajili ulioboreshwa unaowezesha wananchi kupata huduma nyingi kwa njia ya kidijitali kwa urahisi na kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wake, kupitia mfumo huo, wananchi wanaweza kuwasilisha maombi ya huduma, kupakia nyaraka na kufuatilia hatua za maombi yao kwa njia ya mtandao bila kufika ofisini, jambo linalopunguza gharama na kuokoa muda.
"Lengo la maboresho haya ni kurahisisha upatikanaji wa huduma. Mteja anaweza kufanya usajili akiwa nyumbani, ofisini au popote alipo kupitia mfumo wa kidijitali," amesema.
Mwasakafyuka ameongeza kuwa mfumo huo umeimarisha pia uwazi na usalama wa taarifa za kampuni, ambapo wanahisa hupata taarifa kila kunapofanyika mabadiliko yanayohusu umiliki au taarifa nyingine muhimu za kampuni husika.
Amefafanua kuwa ili kutumia huduma hizo kwa ufanisi, mwananchi anatakiwa kuwa na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya simu inayotumika pamoja na anuani sahihi ya barua pepe.
Aidha, amewataka wakulima na wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Nane Nane kutumia fursa hiyo kurasimisha biashara zao, akieleza kuwa hatua hiyo hufungua milango ya kupata mikopo, masoko mapya, zabuni na ushirikiano na taasisi za kifedha na maendeleo.
BRELA ni taasisi inayosimamia usajili na urasimishaji wa biashara nchini ikiwemo usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A. Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nane Nane 2026, taasisi hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuhamasisha ukuaji wa biashara rasmi kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima 'Nane Nane' mwaka 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, "Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."
