Wadau mbalimbali wametembelea Banda la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Maonesho hayo yameanza rasmi Agosti 1,2026 baada ya kufunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.
Kauli mbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka 2026 ni “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050.” Kaulimbiu hii inaakisi umuhimu wa kuwawezesha Watanzania hususan vijana kuwa na maarifa na ujuzi unaochochea uzalishaji wenye tija na maendeleo endelevu ya Taifa.
Katika kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, NACTVET inaendelea kusajili vyuo, kuthibiri ubora wa elimu na kuratibu taasisi zinazotoa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ikiwemo vyuo vinavyotoa kozi za kilimo na mifugo pamoja na shule za sekondari za amali zenye fani hizo.
Kupitia taasisi hizi, vijana wanapata maarifa na ujuzi unaowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji, kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo na mifugo, ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa Taifa.
Tembelea Banda la NACTVET ujifunze zaidi kuhusu fursa za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, na namna zinavyochangia kujenga rasilimali watu yenye ujuzi kwa maendeleo ya taifa.





