Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Wakulima nchini wametakiwa kuwa makini wanaponunua mbegu za mazao kwa kuhakikisha zinakuwa na lebo ya uthibitisho kutoka Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), ili kujiepusha na matumizi ya mbegu bandia zinazoweza kusababisha hasara na mavuno duni.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, jijini Dodoma.
Chimagu amesema lebo ya TOSCI ndiyo uthibitisho rasmi kuwa mbegu husika zimekaguliwa na kuthibitishwa kukidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa kabla ya kuuzwa kwa wakulima.
"Tunataka kuwakumbusha wakulima wetu kuwa kila mfuko wa mbegu unapaswa kuwa na lebo ya TOSCI. Kama haipo, basi usinunue. Hiyo ndiyo njia pekee ya kujikinga na mbegu bandia," amesema.
Amesema serikali imeweka mfumo wa kisasa unaowawezesha wakulima kuhakiki ubora wa mbegu kwa kutumia simu za mkononi, ambapo wanaweza kuthibitisha kwa urahisi kama mbegu walizonunua ni halali au bandia.
Aidha, amewatahadharisha wakulima dhidi ya matumizi ya mbegu zisizothibitishwa, akieleza kuwa mara nyingi husababisha uzalishaji mdogo, kupoteza mtaji na kushusha tija ya kilimo.
Kwa mujibu wa Chimagu, TOSCI inatumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora, kufuata taratibu sahihi za usafirishaji wa mbegu na kuzingatia sheria zinazosimamia biashara ya mbegu nchini.
Amesema matumizi ya mbegu bora yanachangia kwa kiwango kikubwa kuongeza uzalishaji, akibainisha kuwa tafiti zinaonyesha mkulima anayetumia mbegu bora pamoja na mbinu sahihi za kilimo anaweza kuvuna kati ya tani tano hadi 10 kwa hekta, kutegemeana na aina ya zao na mazingira ya uzalishaji.
"Nanenane ni darasa kwa wakulima. Tunawahimiza kutumia fursa hii kujifunza kuhusu mbegu bora na teknolojia mpya za kilimo zitakazowawezesha kuongeza mavuno katika msimu wa kilimo wa 2026/2027. Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo chenye tija na chenye kutumia teknolojia za kisasa," amesema Chimagu.
