Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Ushirika imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Kijiji cha Ushirika katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane 2026 yanayofanyika Nzuguni, jijini Dodoma, ili kujifunza kuhusu fursa zinazotolewa na sekta ya ushirika katika kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Msajili wa Vyama vya Ushirika, Consolata Kiluma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea ufunguzi wa maonesho hayo.
Kiluma amesema Kijiji cha Ushirika kitafunguliwa rasmi Agosti Mosi na kitawakutanisha waoneshaji wapatao 90 kutoka katika vyama mbalimbali vya ushirika nchini, ikiwemo vyama vya mazao ya kilimo, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) pamoja na vyama vya aina nyingine.
Amesema mbali na vyama vya ushirika, kijiji hicho kitashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Benki ya Ushirika, Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), taasisi za bima pamoja na washirika wa maendeleo.
"Wananchi watapata nafasi ya kuona bidhaa na huduma zinazotolewa na vyama vya ushirika, lakini pia kujifunza elimu ya ushirika na namna unavyochangia maendeleo ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla," amesema Kiluma.
Ameeleza kuwa Agosti 3 itakuwa Siku Maalumu ya Ushirika, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika siku hiyo kutakuwa na uzinduzi wa makubaliano mbalimbali kati ya vyama vya ushirika na taasisi washirika pamoja na kuzinduliwa kwa taarifa muhimu zilizokuwa zikiandaliwa kwa muda mrefu.
Aidha, Agosti 6 kutafanyika kongamano maalumu la wanawake wanaoshiriki katika vyama vya ushirika, huku wanawake wengine wakihimizwa kushiriki ili kubadilishana uzoefu na kujadili fursa za kiuchumi kupitia ushirika.
Kiluma amesema sekta ya ushirika imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, ikichangia uuzaji wa mazao makubwa ya kimkakati kwa bei shindani, kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati pamoja na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato yake kwa ufanisi.
Ameongeza kuwa vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati, utoaji wa mikopo kupitia SACCOS, uundaji wa ajira na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jamii katika sekta za afya na elimu.
Kwa mujibu wa Kiluma, mafanikio hayo yanaonesha kuwa ushirika umeendelea kuwa chombo muhimu cha kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza maendeleo jumuishi nchini.


