MWIGULU AITAKA TADB KUONGEZEWA MTAJI KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KILIMO

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kukaa pamoja na Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kujadili namna ya kuongeza mtaji wa benki hiyo, kwa lengo la kuiwezesha kufadhili kwa kiwango kikubwa zaidi sekta za uzalishaji nchini.


Dkt. Nchemba ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 1, 2026, alipotembelea banda la TADB katika uzinduzi wa Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma. Waziri Mkuu alikuwa ameambatana na mawaziri wa wizara husika pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.


Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Nchemba amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kukuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, huku akisisitiza kuwa TADB ina nafasi muhimu ya kufanikisha azma hiyo kupitia utoaji wa mikopo na huduma za kifedha kwa wadau wa sekta hizo.


Aidha, amesema Tanzania bado hutumia takribani dola za Marekani milioni 200 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kila mwaka, hali inayopunguza fedha za kigeni na kudhoofisha ukuaji wa viwanda vya ndani.


Kutokana na hali hiyo, amehimiza kuongezwa kwa uzalishaji wa mazao ya mafuta nchini ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani, kuongeza thamani ya mazao, kuchochea mzunguko wa fedha katika uchumi na kuendelea kufungua fursa za ajira kwa vijana.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.


Amesema hadi sasa TADB imetoa zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya kufadhili miradi ya umwagiliaji, huku ikiendelea kusaidia uzalishaji wa mazao ya biashara ikiwemo kahawa kupitia vyama vya ushirika katika mikoa ya Kagera na Kigoma.


Nyabundege ameongeza kuwa TADB itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta za uzalishaji zinapata rasilimali za kifedha zinazohitajika ili kuongeza tija, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa taifa.


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ndiyo mdhamini mkuu wa Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane mwaka 2026, yanayofanyika chini ya kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko; Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."




Previous Post Next Post