Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Mtandao wa Mashirika Yanayojishughulisha na Utunzaji wa Bionuai Tanzania (TABIO) umeendelea kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kutumia mbegu za asili pamoja na mifugo ya asili, ikiwemo ng'ombe na kuku wa kienyeji, kama njia ya kuimarisha usalama wa chakula na kulinda mazingira nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliofanyika katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa jijini Dodoma, Mratibu wa TABIO, Abdullah Ramadhan Mkindi, alisema mkutano huo umejadili namna ya kuendeleza utunzaji wa mbegu za asili, kuongeza matumizi yake katika uzalishaji wa chakula na kuhamasisha mamlaka husika kutoa msaada kwa wakulima.
Mkindi alieleza kuwa wadau hao pia wamejadili matumizi ya pembejeo rafiki kwa mazingira, ikiwemo viuatilifu vya asili vinavyosaidia kudhibiti visumbufu vya mimea bila kuacha mabaki yenye madhara kwa afya ya binadamu na mazingira baada ya matumizi yake shambani.
Kwa upande wake, Mratibu wa Utafiti na Masuala ya Kisera kutoka Swiz Aid Tanzania, Gladness Martine, alisema ushiriki wa taasisi hiyo katika mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya kilimo ili kuwasaidia wakulima kuhifadhi mbegu za asili na kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

