Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuathiri uzalishaji wa kilimo nchini, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linaendelea kutekeleza mradi wa Climate Change Resilience for Tanzania's Agricultural VET Ecosystem (CREATE) unaolenga kuimarisha ubora wa mafunzo ya kilimo na kuwaandaa wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo.
Mtaalamu wa Miradi wa NACTVET, Christopher Musiba Majigo, amesema mradi huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano na taasisi kutoka Hispania, Italia na Ubelgiji, huku NACTVET ikiwa msimamizi mkuu wa utekelezaji nchini Tanzania.
Amesema kwa sasa mradi huo unatekelezwa katika Chuo cha Kilimo na Mifugo Kilacha mkoani Kilimanjaro na Chuo cha Kilimo Dabaga mkoani Iringa, ambapo vyuo hivyo vinatarajiwa kuwa vituo vya mfano vya kueneza mbinu na teknolojia mpya kwa taasisi nyingine za mafunzo ya kilimo nchini.
Majigo amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuwajengea uwezo wakufunzi kupitia mafunzo maalumu yaliyofanyika nchini Italia na Ubelgiji, yaliyowawezesha kujifunza mbinu za kisasa za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi ili maarifa hayo yawafikie wanafunzi na wakulima.
Aidha, amesema mradi huo umeboresha mitaala ya mafunzo na kuandaa kozi fupi tano zitakazotumika katika vyuo vya kilimo na mifugo, hatua inayolenga kuongeza ujuzi wa vitendo na kuimarisha ubora wa wahitimu wa sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Majigo, mradi wa CREATE ulioanza mwaka 2025 na unaotarajiwa kukamilika mwaka 2027, pia unalenga kuwawezesha vijana kujiajiri na kuongeza fursa za ajira kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu bunifu za uzalishaji wa kilimo.
Ameongeza kuwa vyuo vinavyoshiriki tayari vimeanza kupokea vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia, ambavyo vitasaidia kuboresha mazingira ya mafunzo na kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo.
