TADB YAONGEZA NGUVU YA VIWANDA VYA MAFUTA YA KULA, UZALISHAJI WAPAA MARA 20


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kujitokeza kama chachu ya mageuzi ya sekta ya kilimo nchini baada ya uwekezaji wake kuwezesha kuanzishwa na kupanuliwa kwa viwanda vya uchakataji wa mazao, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.


Mafanikio hayo yamejitokeza wakati Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta na kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo ili kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mafuta ya kula.


Hayo yalibainishwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipotembelea banda la TADB na kupokea taarifa kuhusu mchango wa benki hiyo katika kufadhili miradi ya kilimo na viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao.


Akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Makamu wa Rais alielezwa na Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Mkani Waziri, kuwa benki hiyo imeendelea kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji wa sekta ya kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija, usalama wa chakula na maendeleo ya viwanda vya kuchakata mazao.


Alisema uwekezaji huo umewezesha biashara nyingi za kilimo kukua kutoka uzalishaji wa kawaida hadi viwanda vya kisasa vinavyoongeza thamani ya mazao, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kutoa ajira kwa wananchi.


Ushuhuda wa mafanikio ya uwekezaji huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Kula cha Trolle Meesle, Daniel Amulike, aliyesema ufadhili wa TADB umeibadilisha kampuni hiyo kutoka uzalishaji wa tani 30 hadi tani 624 za mafuta safi ya kula kwa mwezi.


Alisema ongezeko hilo limeiwezesha kampuni kununua mazao mengi zaidi kutoka kwa wakulima wa ndani, kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula na kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali za kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.


"Baada ya kufadhiliwa na TADB tumetoka kuzalisha tani 30 kwa mwezi hadi kufikia tani 624 za mafuta safi ya kula kwa mwezi kupitia kiwanda cha kisasa," alisema Amulike.


Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema Serikali itaendelea kuimarisha uzalishaji wa mazao ya mafuta pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji ili kuongeza kiwango cha kujitosheleza kwa mafuta ya kula nchini.


Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kifedha kama TADB una nafasi muhimu katika kuharakisha mageuzi ya sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko ya wakulima, kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha uchumi wa taifa.


Kwa mafanikio hayo, TADB inaendelea kuthibitisha nafasi yake kama benki kinara katika kufadhili maendeleo ya kilimo na agro-viwanda, huku ikiunga mkono dira ya Serikali ya kujenga uchumi unaotegemea uzalishaji, uchakataji wa mazao na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.




Previous Post Next Post