Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) unashiriki Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ukitumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake na mchango wake katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Ubora wa Mafuta wa PBPA, Datson Mwantuke, alisema Wakala unatoa elimu kuhusu jukumu lake la kuratibu uagizaji na upokeaji wa mafuta kwa pamoja, kusajili Kampuni za Uuzaji wa Mafuta (OMCs), kuhakiki kampuni zinazotaka kusambaza mafuta nchini pamoja na kusimamia mchakato wa zabuni za uagizaji wa mafuta.
Alieleza kuwa wananchi pia wanapata fursa ya kufahamishwa kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kisasa wa SCADA, unaoiwezesha Serikali kufuatilia kwa wakati halisi kiasi cha mafuta kinachoingia nchini kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, hatua inayoongeza uwazi na ufanisi katika usimamizi wa sekta ya mafuta.
Mwantuke alisema PBPA inaendelea kutoa elimu kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja na faida zake, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha kwa wakati, kuongeza ushindani na uwazi katika mchakato wa uagizaji, pamoja na kuimarisha usalama wa nishati nchini.
Aidha, alisema ushiriki wa PBPA katika Maonesho ya Nanenane unalenga kuimarisha mawasiliano kati ya Wakala na wananchi pamoja na wadau mbalimbali, kupokea maoni yao na kutoa ufafanuzi kuhusu huduma na shughuli zinazotekelezwa na taasisi hiyo.
Wananchi wamehimizwa kutembelea banda la PBPA katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ili kupata elimu zaidi kuhusu majukumu ya Wakala na mchango wake katika kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo imara na wa uhakika wa upatikanaji wa mafuta.




