Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuelekeza uwekezaji wake kimkakati katika maeneo ya kipaumbele ya Serikali kwenye sekta ya kilimo ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya sekta hiyo, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ajira kwa Watanzania wengi.
Balozi Omar alitoa maelekezo hayo leo baada ya kutembelea na kukagua banda la TADB katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri huyo alisema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika TADB, hatua iliyowezesha mtaji wa benki hiyo kuongezeka kutoka shilingi bilioni 60 hadi zaidi ya shilingi bilioni 400 ndani ya kipindi kifupi.
Alisema TADB ina nafasi muhimu katika kuchochea mageuzi ya sekta ya kilimo kupitia utoaji wa mitaji na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Balozi Omar alieleza kuwa kufikiwa kwa uchumi wa dola trilioni moja kunategemea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu, ambazo zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kuimarisha sekta hiyo kwa lengo la kupunguza umaskini na kuongeza kipato cha Mtanzania hadi kufikia wastani wa dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.
Waziri huyo pia aliwapongeza wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo kwa ubunifu wao na ubora wa bidhaa wanazozalisha, akisema bidhaa nyingi zina viwango vinavyokubalika lakini bado hazijapata nafasi ya kutosha katika masoko.
Kutokana na hali hiyo, aliiagiza Wizara ya Kilimo kuendelea kusaidia kutangaza bidhaa hizo na kuwawezesha wazalishaji kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
"Nawapongeza Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tuendelee kushirikiana kwa karibu ili kuleta maendeleo makubwa zaidi katika sekta hii," alisema.
Akizungumzia sekta ya mifugo, Balozi Omar alisema bado inahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha ili kuongeza ufanisi wake, akibainisha kuwa ni sekta yenye faida kubwa na inayoweza kurejesha haraka fedha zinazowekezwa.
Kwa upande wa sekta ya uvuvi, alisema inaendelea kufanya vizuri na kuvutia wananchi wengi kujiingiza katika shughuli za uzalishaji, hivyo inahitaji kupewa kipaumbele zaidi ili kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
