Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Wakati sekta ya mifugo ikiendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, wataalamu wamewataka wafugaji kubadili mtazamo na kuanza kuona ngozi za mifugo kama rasilimali yenye thamani kubwa badala ya bidhaa inayopuuzwa. Elimu hiyo imeendelea kutolewa katika Maonesho ya Nanenane, ambapo Chuo cha VETA Dakawa kinatumia jukwaa hilo kuwafikia wafugaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mwalimu wa bidhaa za ngozi kutoka Chuo cha VETA Dakawa kilichopo mkoani Morogoro, Hamidu Shabani, amesema maonesho hayo yamekuwa fursa adhimu ya kuwaelimisha wafugaji kuhusu umuhimu wa kutunza ngozi za mifugo kuanzia hatua za ufugaji hadi baada ya kuchinjwa, ili kuongeza ubora wa bidhaa hiyo na kuinua kipato chao.
Amesema kuwa mbali na kuonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa ngozi, ikiwemo viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zenye thamani, VETA Dakawa inaendelea kutoa elimu ya kitaalamu kuhusu mbinu bora za ufugaji zinazosaidia kupata ngozi safi na zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.
Kwa mujibu wa Hamidu, changamoto kubwa inayowakabili wafugaji wengi si idadi ya mifugo waliyonayo, bali ni namna wanavyoitunza. Alieleza kuwa baadhi yao hutengeneza mazizi kwa kutumia miba au nyaya zenye ncha kali ambazo husababisha mifugo kupata mikwaruzo na majeraha yanayoharibu ubora wa ngozi.
Alifafanua kuwa ngozi yenye mikwaruzo hupoteza thamani yake mara moja sokoni, hali inayosababisha wafugaji kukosa mapato ambayo wangeweza kuyapata kama wangetunza mifugo yao kwa kufuata kanuni za kitaalamu. Amesisitiza kuwa utunzaji mzuri wa ngozi huanza tangu mnyama akiwa hai.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wafugaji kujenga mabanda ya mbao au kutumia vifaa visivyo na ncha kali vinavyoweza kusababisha majeraha kwa mifugo. Pia aliwashauri kuweka alama za utambulisho wa mifugo chini ya goti badala ya sehemu nyingine za mwili, ili kulinda ubora wa ngozi ambayo ndiyo malighafi muhimu ya viwanda vya bidhaa za ngozi.
Hamidu amesema kuwa ngozi ikitunzwa vizuri inaweza kuongeza thamani kubwa ya mifugo, ambapo mfugaji anaweza kupata kati ya shilingi 300,000 hadi 600,000 zaidi kutokana na ubora wa ngozi na bidhaa zitakazotengenezwa baada ya kuchakatwa. Hivyo, aliwataka wafugaji kutambua kuwa ngozi si taka, bali ni mali yenye uwezo wa kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Aidha, amewahimiza wafugaji kutumia elimu inayotolewa na wataalamu wa VETA na taasisi nyingine za mifugo ili kuongeza tija katika uzalishaji, kuboresha ubora wa ngozi na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko mbalimbali.
Akizungumzia hali ya soko, Hamidu amesema mahitaji ya bidhaa za ngozi yanaendelea kuongezeka, huku VETA Dakawa ikiendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutengeneza bidhaa bora na kutoa mafunzo yanayochochea ukuaji wa sekta hiyo. Amesema ushirikiano kati ya wafugaji, wataalamu na wadau wa viwanda vya ngozi utakuwa chachu ya kuongeza thamani ya mifugo, kufungua ajira na kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta ya ngozi.
