Na Edward Winchislaus, Dodoma.📍
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora ni msingi wa kuongeza tija na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamesemwa leo Agosti 5,2026 na Meneja wa TBS Kanda ya Kati Bw. Hamisi Mwanasala wakati akizungumza katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yenye kaulimbiu isemayo "Tambua Soko:Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa 2050."
Mwanasala amesema TBS ni miongoni mwa wadau wakuu wanaotekeleza kaulimbiu hiyo kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia viwango vinavyotakiwa akieleza kuwa bidhaa yoyote inayolenga kutambulika na kudumu sokoni lazima iwe na ubora uliothibitishwa na TBS.
Amesema kuzingatia viwango vya ubora huongeza tija kwa wazalishaji, huongeza mapato ya viwanda na wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa hivyo kuifanya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kufikiwa kwa urahisi zaidi.
Kwa mujibu wa Mwanasala TBS inaendelea kutoa huduma mbalimbali zikiwemo ukaguzi wa viwanda, upimaji wa sampuli, usajili wa bidhaa na utoaji wa leseni ya matumizi ya Alama ya Ubora ya TBS. Ameongeza kuwa huduma hizo sasa zinapatikana kupitia ofisi za kanda tofauti na ilivyokuwa awali ambapo zilipatikana katika makao makuu ya Dar es Salaam pekee.
Amesema shirika limeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma kwa kuwa na maabara ya kisasa Dodoma huku ujenzi wa maabara nyingine ukiendelea katika mikoa ya Mwanza na Arusha sambamba na kuongeza watumishi na vitendea kazi ili kuimarisha utoaji wa huduma.
Akizungumzia maonesho hayo, Mwanasala amesema TBS inatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ubora wa bidhaa na kutatua changamoto mbalimbali zinazowasilishwa.
"Tunayo timu ya wataalamu wa TBS Kanda ya Kati wanatembelea mabanda ya wazalishaji ili kuwafikia wale ambao bado hawajapata nembo ya Ubora ya TBS na kuwapa elimu kuhusu taratibu za kupata ithibati hiyo",ameeleza.
Hata hivyo amesema TBS imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali kupitia mifumo ya kielektroniki inayorahisisha usajili wa maombi, utoaji wa huduma na mawasiliano kati ya shirika na wateja.
Vilevile amesema TBS hufanya ukaguzi wa viwanda zaidi ya mara nne kwa mwaka pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizopo sokoni ili kuhakikisha zinaendelea kukidhi viwango vinavyotakiwa. Ameongeza kuwa kila malalamiko yanayowasilishwa hushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Sura ya 130 huku hatua za kisheria zikichukuliwa kwa yeyote anayebainika kukiuka sheria hiyo.
