Kongwa, Dodoma Julai 24, 2026📍
Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Mhe. Angela Kairuki, amefanya ziara ya siku mbili katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mhe. Kairuki amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea thamani halisi ya fedha zilizowekezwa na Serikali, ubora wa miradi pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Saimoni Mayeka, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Omary Nkuro, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Jesca Mbogo, pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Aidha, ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Dodoma chini ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Rosemary Senyamule, kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema umechangia kuboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo.
Katika sekta ya afya, Waziri Kairuki amepongeza ujenzi wa vituo 11 vya afya katika Wilaya ya Kongwa ambavyo vimekamilika kwa muda mfupi na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Pia ameweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Kongwa na kueleza kuwa miradi hiyo imeongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa zaidi ya wakazi 28,000 huku ikipunguza msongamano katika hospitali.
Ametoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha vifaa tiba vilivyoidhinishwa vinapatikana kwa wakati ili vituo hivyo viweze kutoa huduma kwa ufanisi. Vilevile amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya.
Akizungumzia sekta ya elimu, Waziri Kairuki amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu kupitia mpango wa Elimu Bila Ada, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 1.1 zimetengwa kwa elimu ya msingi na bilioni 1.5 kwa elimu ya sekondari.
Amesema Wilaya ya Kongwa imenufaika na ujenzi wa shule 26, madarasa 640, maabara 50 za sayansi pamoja na nyumba 176 za walimu, hatua iliyoboa mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Pia amempongeza Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Jesca Mbogo, kwa kuwasilisha ombi la kompyuta za kufundishia, huku akiahidi kufuatilia upatikanaji wa kompyuta 42 kwa shule mbili zilizobaki ili kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika elimu.
"Tunataka watoto wote wapate fursa ya elimu bora. Serikali inaendelea kujenga miundombinu, kuajiri walimu na kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufaulu," amesema Waziri Kairuki.
Katika sekta ya maji, Waziri Kairuki amempongeza Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso, kwa juhudi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia uchimbaji wa visima 19 katika Wilaya ya Kongwa.
Amesema hatua hiyo imeongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo na mifugo, huku Serikali ikiendelea kutoa wataalamu wa kilimo, pembejeo na kuanzisha mashamba darasa ili kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wananchi.
Katika kuimarisha uchumi wa kidijitali, Waziri Kairuki amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za mawasiliano kwa kuongeza upatikanaji wa mitandao ya simu na intaneti, huku kata zote za Wilaya ya Kongwa zikifikishiwa huduma ya umeme, jambo litakalosaidia kukuza biashara, elimu na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Saimoni Mayeka, amemshukuru Waziri Kairuki kwa kutembelea wilaya hiyo na kujionea maendeleo yaliyofikiwa.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 38.6 katika utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, maji na miundombinu wilayani humo.
Mhe. Mayeka amewataka viongozi wa ngazi zote kuendelea kuhamasisha wananchi kutumia teknolojia katika shughuli za kila siku na kuhakikisha huduma za afya, elimu na maendeleo mengine zinaendelea kuboreshwa.
Akihitimisha ziara yake, Waziri Kairuki pia alimkumbuka aliyekuwa Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Wilaya ya Kongwa kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Aidha, amewapongeza wazazi wanaochangia utoaji wa chakula shuleni, akisema ushiriki wao una mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
"Tukishirikiana, tutaendelea kujenga Kongwa yenye afya bora, elimu bora na teknolojia imara kwa maendeleo ya Taifa,"amesema Waziri Kairuki.






