USHIRIKIANO WA JESHI LA POLISI NA CAC WAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA


Na Carlos Claudio, Chamwino.📍


Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto limewataka wananchi kote nchini kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, likisisitiza kuwa ukatili huo hauwezi kumuacha mtu yeyote salama na unapaswa kupingwa kwa nguvu zote.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kigoma, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Michael Mjema, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ufunguzi wa Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo lililofanyika katika viwanja vya Chamwino Arts Centre (CAC), mkoani Dodoma.


Mjema alisema matamasha yanayokusanya watu wengi ni fursa muhimu kwa Jeshi la Polisi kupitia falsafa ya Polisi Jamii kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia.


"Sisi Jeshi la Polisi tunasema ukatili wa kijinsia hauwezi kumuacha mtu salama. Tunatoa wito kwa wananchi waachane na vitendo hivyo ili kujenga jamii salama," alisema.


Alieleza kuwa maafisa wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamekusanyika mkoani Dodoma kwa mkutano mkuu wa kitaifa, huku wakitumia siku tatu za mkutano huo kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu.



Kwa mujibu wake, maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi kuanzia ngazi ya wilaya, tarafa, kata, vijiji hadi vitongoji, ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.


Alisema Tamasha la Muziki wa Cigogo lilichaguliwa kwa makusudi kutokana na uwezo wake wa kuvutia maelfu ya washiriki kutoka Wilaya ya Chamwino, wilaya nyingine za Mkoa wa Dodoma pamoja na mikoa jirani.


"Tuliona huu ni mkusanyiko mkubwa wa wananchi wenye umuhimu wa kupatiwa elimu ya ukatili wa kijinsia. Tumefurahi kuona mwitikio mkubwa wa watu na tunaamini elimu tuliyoitoa itasaidia kujenga jamii salama," alisema.


Mjema alibainisha kuwa elimu iliyotolewa ilihusu maana ya ukatili wa kijinsia, aina zake, madhara yake, umuhimu wa kutoa taarifa mapema, majukumu ya Dawati la Jinsia na Watoto, namna ya kulinda eneo la tukio pamoja na umuhimu wa wananchi kushiriki kutoa ushahidi ili wahusika wa vitendo vya ukatili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.


Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola ni msingi muhimu wa kutokomeza ukatili wa kijinsia, akieleza kuwa lengo la Jeshi la Polisi ni kuona Mkoa wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla vinakuwa maeneo salama yasiyo na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo hatarini.






Previous Post Next Post