Na Carlos Claudio, Chamwino.📍
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka Watanzania kuendelea kuthamini na kushiriki matamasha ya utamaduni yanayolenga kuhifadhi na kurithisha mila na desturi za taifa, likieleza kuwa matamasha hayo ni nguzo muhimu ya kulinda utambulisho wa Tanzania na kukuza vipaji vya wasanii.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Edward Elias Buganga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika hitimisho la Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo lililofanyika katika viwanja vya Chamwino Arts Centre.
Buganga amesema BASATA ilishiriki tamasha hilo kwa lengo la kuungana na wananchi wa Chamwino kusherehekea tukio hilo muhimu ambalo limejikita katika kurithisha vizazi mila, desturi na maadili ya Kitanzania.
"Tamasha hili lina faida kubwa kwa jamii kwa sababu linasaidia kurithisha urithi wa kitamaduni, kuzungumzia maadili ya Kitanzania na kuimarisha mshikamano wa jamii. Hili ni jambo muhimu sana kwetu kama taasisi inayosimamia maendeleo ya sanaa nchini," amesema.
Amesema pamoja na mabadiliko yanayoletwa na sayansi na teknolojia, bado ni muhimu kuhakikisha utamaduni wa Tanzania unalindwa na kuendelezwa kwa kutumia mbinu za kisasa bila kupoteza asili yake.
Buganga amesema Chamwino, ikiwa katika makao makuu ya nchi, ni eneo muhimu katika kukuza na kuendeleza sanaa za asili, huku BASATA ikiendelea kutekeleza wajibu wake wa kuzisimamia na kuzikuza.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kutoa msukumo katika maendeleo ya sekta ya sanaa na kuhakikisha maadili ya jamii ya Kitanzania yanahifadhiwa.
Amesema Tamasha la Muziki wa Cigogo limejidhihirisha kama jukwaa muhimu la kulinda, kukuza na kuendeleza utamaduni wa Wagogo pamoja na urithi wa Kitanzania kwa ujumla.
"Tumeona ngoma za asili, vifaa vya jadi, nyumba za asili na vyombo vilivyokuwa vinatumiwa na jamii ya Wagogo kuhifadhi chakula. Haya yote yanaonesha utajiri wa utamaduni wetu na yanatoa nafasi ya kukuza vipaji vya wasanii," amesema.
Kwa upande wa BASATA, amesema tamasha hilo pia limetoa fursa ya kutambua na kusajili vikundi vya sanaa pamoja na wasanii mmoja mmoja ili waweze kunufaika na mifumo rasmi ya serikali ya kuwawezesha kukuza uchumi, biashara na ajira kupitia sekta ya sanaa.
Amesema usajili huo utasaidia kuweka mazingira bora ya maendeleo ya wasanii na kuongeza fursa za kushiriki katika matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Akihitimisha, Buganga ametoa wito kwa Watanzania kuenzi na kuhifadhi sanaa za asili pamoja na kutumia teknolojia za kidijitali kuzihifadhi na kuzitangaza ndani na nje ya nchi ili urithi wa Tanzania uendelee kutambulika duniani.


