VETA YAWAKARIBISHA VIJANA KUSOMEA UFUNDI NA UJASIRIAMALI SABASABA


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kimewaomba Watanzania kuwapeleka vijana wao kusomea fani mbalimbali za ufundi stadi, ili waweze kupata maarifa yatakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo yao.


Wito huo umetolewa na Mwalimu wa Ufundi wa Selemala kutoka VETA, Ayubu Omari, wakati akitoa elimu kwa waandishi wa habari waliotembelea banda la VETA katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Omari amesema VETA imejikita katika kuwapa vijana stadi za maisha kupitia mafunzo ya fani mbalimbali, sambamba na elimu ya ujasiriamali inayowaandaa kutumia maarifa yao kuanzisha shughuli za kiuchumi.


Amesema maonesho hayo yanafanyika chini ya kauli mbiu inayosisitiza fahari ya Mtanzania, huku VETA ikitumia fursa hiyo kuonesha namna ambavyo mafunzo ya ufundi yanavyoweza kuwa suluhisho la changamoto ya ajira kwa vijana.



“Kwa upande wangu ninafundisha fani ya uselemala. Tunatoa kozi ndefu ya miaka miwili pamoja na kozi fupi zinazochukua kati ya miezi mitatu hadi sita,” amesema Omari.


Amesema katika maonesho ya mwaka huu, VETA imeonesha bidhaa mbalimbali za samani zilizotengenezwa kwa kutumia miti, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya malighafi za ndani katika uzalishaji wa samani bora.


Miongoni mwa bidhaa hizo ni disabled toilet stool, kifaa maalum kilichobuniwa kumsaidia mtu mwenye ulemavu wa miguu ambaye anapata changamoto ya kujisaidia akiwa chooni.


“Stool hii inalenga kumrahisishia Mtanzania mwenye changamoto ya miguu kuweza kujisaidia kwa urahisi na usalama,” amesema.


Pia, VETA imeonesha expansion showcase, kabati maalum linaloweza kupanuliwa kulingana na ukubwa wa chumba au nyumba ya mtumiaji.


Omari amesema kabati hilo limekusudiwa kuwasaidia wananchi wanaoanza maisha katika vyumba vidogo, ambapo wanaweza kulipanua kadiri wanavyopiga hatua kiuchumi na kuhamia katika makazi yenye nafasi kubwa zaidi.


Amesema kabati hilo limetengenezwa kwa mbao maalum zinazodumu kwa muda mrefu na zisizoshambuliwa kwa urahisi na mchwa.


Kwa mujibu wa Omari, mwanafunzi anapojiunga na VETA hafundishwi tu kutengeneza samani au kufanya kazi za ufundi, bali pia hupewa maarifa ya ujasiriamali yatakayomwezesha kutumia taaluma yake kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali.

🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA
Previous Post Next Post