Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe kimebuni mashine maalumu ya kuwasaidia wajasiriamali kujaza bidhaa mbalimbali kwa kipimo sahihi, hatua inayolenga kuongeza usafi, ubora na thamani ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali.
Ubunifu huo umeoneshwa katika banda la VETA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Akitoa elimu kwa waandishi wa habari waliotembelea banda hilo, Mwalimu wa Ufundi wa Umeme wa Viwanda kutoka VETA Chang’ombe, Athuman Pazzi, amesema mashine hiyo imeundwa kutokana na changamoto inayowakabili wajasiriamali wengi wanapofikia hatua ya kujaza bidhaa zao kwenye vifungashio.
Amesema wajasiriamali wengi wana vifaa bora vya kutengeneza bidhaa, ikiwemo mashine za kuchanganya sabuni za maji na mafuta, lakini hukumbana na changamoto ya kujaza bidhaa hizo kwa kutumia mikono, mirija, majagi na beseni.
Kwa mujibu wa Pazzi, utaratibu huo unaweza kupunguza usafi wa bidhaa, kusababisha upotevu wa malighafi na kushusha thamani ya bidhaa mbele ya wateja.
“Tumefanya utafiti na kubaini kuwa wengi wanatumia njia za kawaida za kujaza bidhaa, hali ambayo inaweza kuathiri ubora na muonekano wa bidhaa zao.
Kupitia mafunzo ya ufundi stadi, wanafunzi wa fani za fundi bomba na umeme waliinuka na kubuni mashine hii kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye karakana zetu,” amesema.
Ameeleza kuwa mashine hiyo humwezesha mjasiriamali kuweka kiwango cha ujazo anachohitaji kabla ya kuanza kujaza bidhaa kwenye vifungashio, hivyo kuhakikisha kila kifungashio kinapata kiasi kinachofanana.
Pazzi amesema mashine hiyo inatumia umeme wa kawaida wa nyumbani, jambo linaloifanya kuwa rahisi kutumiwa na wajasiriamali wa ngazi mbalimbali, hususan wanaojishughulisha na uzalishaji wa sabuni za maji, mafuta na bidhaa nyingine zinazohitaji kujazwa kwa vipimo maalumu.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda la VETA ili kujionea teknolojia na bunifu mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
“Tunawaalika wazazi na walezi kuwaleta vijana wao VETA, kwa sababu mafunzo ya ufundi stadi ni sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira kwa vijana. Vijana wanapata ujuzi wa kujiajiri na pia kuanzisha bunifu zinazotatua changamoto za jamii,” amesema.

