BRELA YAHIMIZA WAJASIRIAMALI KULINDA BIASHARA ZAO KWA KUSAJILI ALAMA NA MAJINA YA BIASHARA



Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wajasiriamali nchini kutumia huduma za usajili wa majina ya biashara na alama za biashara ili kulinda bidhaa zao, kuongeza ushindani wa haki sokoni na kuendesha biashara kwa mujibu wa sheria.


Wito huo umetolewa Julai 10, 2026 na Ofisa Usajili wa BRELA, Benedickson Wilson, wakati akitoa mafunzo kwa wajasiriamali wanawake katika banda la Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) pamoja na banda la Wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).


Wilson alisema usajili wa alama za biashara ni hatua muhimu inayompa mmiliki haki ya kipekee ya kutumia alama yake na kumlinda dhidi ya watu wanaoweza kuitumia au kusajili alama zinazofanana na kusababisha mkanganyiko kwa watumiaji.


Alieleza kuwa mfumo wa usajili wa alama unazingatia madaraja 45 ya bidhaa na huduma, ambapo kila biashara husajiliwa katika daraja husika kulingana na shughuli zake. Alitolea mfano kuwa bidhaa za vipodozi husajiliwa katika Daraja la 3.



"Baada ya kusajili alama, mmiliki anapata ulinzi wa kisheria na anaweza kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayetumia alama hiyo bila idhini au kusajili alama inayofanana," alisema Wilson.


Aliongeza kuwa usajili wa alama za biashara husaidia kujenga utambulisho wa bidhaa au huduma, kuongeza imani kwa wateja na kuimarisha ushindani wa biashara huku ukiwalinda watumiaji dhidi ya bidhaa zinazoweza kuleta mkanganyiko sokoni.


Kwa upande wao, baadhi ya wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara zao na kulinda chapa zao kupitia BRELA.


Mjasiriamali Melania Shawa alisema hapo awali hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu huduma za BRELA, lakini kupitia mafunzo hayo amefahamu kuwa usajili wa jina la biashara unaweza kukamilika ndani ya siku moja na kumpatia cheti cha usajili.


BRELA inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kutoa elimu kwa umma na huduma mbalimbali kupitia mabanda yake mawili, huku ikiwakaribisha wananchi na wafanyabiashara kutembelea mabanda hayo ili kupata ushauri na huduma za usajili kabla ya kuhitimishwa kwa maonesho hayo Julai 13, 2026.





Previous Post Next Post