CAC YAPONGEZWA KWA KUENDELEZA UTAMADUNI, SERIKALI YAHAIDI USHIRIKIANO ZAIDI


Na Carlos Claudio, Chamwino, Dodoma.📍


Serikali imeipongeza Chamwino Arts Centre (CAC) kwa mchango wake mkubwa wa kuhifadhi na kurithisha utamaduni wa ngoma za asili kwa vizazi mbalimbali, huku ikiahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili taasisi hiyo ifikie malengo yake ya kukuza sanaa, utamaduni na maendeleo ya jamii.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, wakati wa ufunguzi wa Tamasha la 17 la Chamwino Music Festival lililofanyika katika viwanja vya Chamwino Arts Centre (CAC).



Mhe. Mayanja alisema Serikali imefurahishwa na namna tamasha hilo linavyowakutanisha watu wa rika zote kushiriki na kujifunza ngoma za asili, jambo linaloonyesha kuwa utamaduni unaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.


"Hata katika maonesho tumeona kuna ngoma zinazochezwa na watu wazima, vijana na hata watoto wadogo. Hii inaonyesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha utamaduni wetu unaendelea kuishi. Tunawapongeza sana Chamwino Arts Centre kwa maono haya makubwa," alisema.


Alibainisha kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na CAC kwa miaka mingi katika kufanikisha tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwezi Julai, akisisitiza kuwa taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi mila na desturi za wananchi wa Dodoma kupitia sanaa za maonesho.


Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, wananchi wa Dodoma wameendelea kuwa mfano wa kuhifadhi utamaduni wao kwa kutumia burudani za ngoma za asili, hali ambayo imeendelea kuimarishwa kupitia shughuli mbalimbali zinazoandaliwa na CAC.



Aidha, aliwapongeza wadau wote wanaoendelea kuunga mkono tamasha hilo, akieleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo "Sanaa Yetu, Nishati Yetu" imeongeza thamani ya tamasha kwa kuunganisha sanaa na elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Alisema kupitia mkusanyiko mkubwa wa wananchi, Serikali inaamini elimu kuhusu matumizi ya nishati safi itawafikia wananchi wengi, hususan wanaotoka maeneo ya vijijini, na hivyo kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi.


"Tunawapongeza kwa maono haya makubwa ya kutumia sanaa kama jukwaa la kutoa elimu kwa jamii. Serikali itaendelea kushirikiana na Chamwino Arts Centre ili kuhakikisha malengo haya yanatimia kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla," alisisitiza.









Previous Post Next Post