SUMAJKT YAPONGEZWA KWA KUTOA AJIRA KWA VIJANA


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho (Mb), amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali, SUMAJKT, kwa mchango wake katika kutoa ajira kwa vijana na kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.


Dkt. Nyansaho alitoa pongezi hizo Julai 6, 2026, alipofanya ziara katika banda la JKT kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba, yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.


Alisema kampuni tanzu za SUMAJKT zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuwapatia vijana fursa za ajira, sambamba na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali.


Akitoa mfano, Waziri huyo alisema Kampuni ya Usafi na Unyunyizi Dawa ya SUMAJKT, inayojulikana kama SUMAJKT Cleaning and Fumigation Company Limited, imefanikiwa kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 4,000 Watanzania.


“JKT kupitia SUMAJKT limeendelea kuonyesha namna taasisi za umma zinavyoweza kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na utoaji wa ajira kwa vijana, jambo ambalo ni muhimu katika kupunguza ombwe la ajira nchini,” alisema Dkt. Nyansaho.


Katika hatua nyingine, Dkt. Nyansaho amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na JKT kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kulinda taifa na kushiriki katika uzalishaji mali.


Alisema mchango wa majeshi hayo unaendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha nchi inabaki salama, huku wananchi wakipata mazingira ya amani na utulivu wa kutekeleza shughuli zao za maendeleo.


Aidha, Waziri huyo amewahamasisha wananchi kutembelea banda la JKT katika maonesho hayo ili kujifunza zaidi kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na jeshi hilo kupitia vikosi, makambi, shule, chuo pamoja na huduma na biashara zinazotolewa na kampuni tanzu za SUMAJKT.

Previous Post Next Post