NAIBU WAZIRI JAFARI SEIF AWAHIMIZA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LA TAMISEMI SABASABA


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Jafari Seif, amewataka wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani kutembelea banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), akisema huduma zinazotolewa kupitia kituo cha huduma cha pamoja (One Stop Centre) zimekuwa zikitatua changamoto za wananchi kwa haraka na ufanisi.


Akizungumza alipotembelea banda la TAMISEMI katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Dkt. Seif alisema wananchi wanaofika katika banda hilo wanapata huduma mbalimbali za Serikali chini ya eneo moja, jambo linalowaondolea usumbufu wa kutembea katika ofisi nyingi kutafuta huduma.



Alisema One Stop Centre imekuwa ikipokea na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazohusu huduma za mamlaka za serikali za mitaa, huku wataalamu kutoka idara na taasisi zilizo chini ya TAMISEMI wakitoa majibu na ufumbuzi wa papo kwa papo.


"Niwaombe wananchi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani wajitokeze kwa wingi kutembelea banda letu. Hapa wanapata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata huduma mbalimbali kwa wakati mmoja bila usumbufu," alisema Dkt. Seif.


Aidha, alieleza kuwa ushiriki wa TAMISEMI katika maonesho hayo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na wizara pamoja na kupokea maoni yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za umma.


Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yameendelea kuvutia maelfu ya wananchi wanaotembelea mabanda mbalimbali ya taasisi za Serikali na sekta binafsi kujionea bidhaa, huduma na fursa zinazotolewa.

Previous Post Next Post