SOFTENA YAWAHIMIZA WANANCHI KUJIFUNZA AFYA NA MATUMIZI YA BIDHAA ZA NGOZI


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Wananchi wamehimizwa kutembelea banda la Softena Enterprises katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ili kupata elimu kuhusu namna ya kuboresha afya pamoja na matumizi sahihi ya bidhaa mbalimbali za ngozi.


Wito huo umetolewa na mwakilishi wa kampuni hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda la Softena, akieleza kuwa maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kukutana na wananchi, kuwapa elimu na kuwasaidia kufahamu bidhaa zinazoweza kuchangia ustawi wa afya na utunzaji wa ngozi.


Alisema Softena imejikita katika kutoa bidhaa zenye ubora zinazolenga kukidhi mahitaji ya watumiaji, huku ikiendelea kusisitiza matumizi salama ya bidhaa hizo kwa kufuata ushauri wa wataalamu.



Aidha, alibainisha kuwa wageni wanaotembelea banda hilo wanapata nafasi ya kupewa maelekezo ya moja kwa moja kuhusu matumizi ya bidhaa mbalimbali, kupata ushauri kulingana na mahitaji yao na kujionea bidhaa mpya zinazotolewa na kampuni hiyo.


Aliongeza kuwa ushiriki wa Softena katika Maonesho ya Sabasaba ni sehemu ya jitihada za kampuni kusogeza huduma karibu na wananchi, kujenga uelewa kuhusu afya na utunzaji wa ngozi, pamoja na kuimarisha mahusiano na wateja.


Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo walisema wamevutiwa na elimu waliyoipata, wakieleza kuwa imewasaidia kuelewa umuhimu wa kuchagua bidhaa bora za ngozi na kufuata matumizi sahihi kwa ajili ya kulinda afya zao.



Walitoa wito kwa wananchi wengine kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la Softena ili kujifunza zaidi kuhusu afya, utunzaji wa ngozi na bidhaa zinazotolewa na kampuni hiyo.

Previous Post Next Post