NACTVET YAHAMASISHA WAZAZI KUPELEKA WATOTO MAFUNZO YA AMALI


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewataka wazazi, walezi na wadau wa elimu nchini kuwahamasisha watoto kujiunga na mafunzo ya amali, likisema elimu hiyo inawajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kutekeleza kazi kwa vitendo.


Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, leo Julai 6, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba.


NACTVET inashiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kusogeza huduma zake karibu na wananchi, pamoja na kutoa elimu kuhusu uanzishwaji na usimamizi wa taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Akizungumza katika banda la taasisi hiyo, Dkt. 


Lingwanda amesema wananchi wanaotembelea banda la NACTVET wanapata fursa ya kuuliza maswali na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na baraza hilo.


Huduma hizo zinajumuisha ushauri kuhusu namna ya kuanzisha taasisi za elimu ya ufundi, taarifa za uthibitishaji wa vyeti pamoja na huduma nyingine za kiutawala zinazopatikana katika ofisi za NACTVET.


Amesema mwitikio wa wananchi umeendelea kuwa mkubwa, huku rejesta ya wageni ikionyesha kuwa watu wengi wamefika katika banda hilo kupata taarifa na huduma walizokuwa wakizihitaji.



“Tunawakaribisha wananchi wote kutumia fursa ya maonesho haya kufika katika banda letu, kupata taarifa sahihi na huduma mbalimbali zinazotolewa na NACTVET. Pia tunaomba waliotembelea waendelee kuwafikishia wengine ujumbe kuwa bado tupo hapa Sabasaba na tunaendelea kuwahudumia,” amesema.


Mbali na huduma za ushauri na uthibitishaji wa vyeti, NACTVET imetumia maonesho hayo kuonesha umuhimu wa elimu ya amali kwa vitendo kupitia wanafunzi kutoka baadhi ya taasisi zinazotoa mafunzo hayo.


Wanafunzi hao wamekuwa wakionesha ujuzi mbalimbali walioupata darasani, hali inayodhihirisha uwezo wa mafunzo ya amali kuwajenga vijana wanaoelewa walichofundishwa na wenye uwezo wa kukitekeleza katika mazingira halisi ya kazi.


Kwa mujibu wa Dkt. Lingwanda, mafunzo ya amali yana mchango mkubwa katika kutengeneza nguvu kazi yenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uzalishaji na maendeleo ya taifa.


“Tulichokileta hapa ni baadhi tu ya fani zilizopo. Fani ni nyingi, lakini tumetoa mfano wa maeneo machache ili wananchi waone uwezo wa vijana wetu. Inawezekana mwakani tukapanua zaidi na kuonesha fani nyingine,” amesema.


Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi stadi nchini, sambamba na kuwapa vijana wengi zaidi nafasi ya kupata ujuzi utakaowawezesha kuajirika au kujiajiri.


🚨Full Video Inapatikana Katikia YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post