Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, akisema ushiriki huo unaonyesha dhamira ya kutangaza fursa za uwekezaji na ukuaji wa jiji hilo.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Trade Fair Grounds, Shekimweri alisema kila nafasi inayopatikana inapaswa kutumiwa kuitangaza Dodoma kama jiji linalokua kwa kasi na lililo tayari kupokea uwekezaji mkubwa.
Alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, pamoja na Mstahiki Meya, Alimwoni Chaula, kwa usimamizi wa halmashauri na kuendeleza dira ya kukuza jiji hilo.
“Pongezi za dhati kwa Mkurugenzi wa Jiji na Mstahiki Meya kwa kusimamia vizuri halmashauri na dira ya ukuaji wa Jiji la Dodoma. Kila fursa inayopatikana ya kutangaza nafasi ya Dodoma katika ukuaji wake itumike kwa kasi,” alisema Shekimweri.
Aidha, aliipongeza timu ya maafisa wa halmashauri hiyo, ikiwemo maafisa biashara, ardhi na habari, kwa kushiriki kwa pamoja katika maonesho hayo na kutoa maelezo kwa wadau wanaotembelea banda lao.
Shekimweri alisema amefurahishwa na namna Halmashauri ya Jiji la Dodoma inavyonadi fursa mbalimbali zilizopo katika jiji hilo, hususan kwenye sekta ya kilimo na uchakataji wa mazao.
Alitaja fursa katika kilimo cha zabibu, tufaa, alizeti, korosho na matunda mbalimbali, akibainisha kuwa uwekezaji katika uchakataji na kuongeza thamani ya mazao unaweza kuchochea uchumi wa wananchi na jiji kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Shekimweri, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, anaendelea kusisitiza uzalishaji wa tufaa, huku Dodoma ikitarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo makubwa ya uzalishaji wa zao hilo nchini katika siku zijazo.
Kwa upande wake, Neema Fundi kutoka Kampuni ya Dane Wine alisema wamefarijika na ziara ya Mkuu wa Wilaya, akieleza kuwa kutembelewa na viongozi kunawapa motisha washiriki wa maonesho kuendelea kuonesha bidhaa na huduma zao
“Furaha yangu ni kuona viongozi wanapita kutuuliza shughuli tunazofanya na changamoto zinazotukabili. Tumefarijika sana,” alisema Fundi.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.


