Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam.📍
Wananchi wametakiwa kutumia fursa ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba, kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali za kisheria zinazotolewa na wizara hiyo.
Wizara hiyo inashiriki maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kuwapa uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya sheria yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya utatuzi wa Migogoro Wizara ya Katiba na Sheria Felix Chakila amesema tangu walipowasili Juni 28, wamepokea na kuwahudumia takriban wananchi 1,300 waliowasilisha changamoto tofauti za kisheria.
Amesema baadhi ya masuala yaliyojitokeza kwa wingi ni migogoro ya mirathi, ardhi na jinai, huku wananchi wengine wakihitaji mwongozo wa namna ya kufikisha malalamiko yao katika mamlaka sahihi kwa ajili ya kupata ufumbuzi.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, wananchi wanaofika katika banda hilo wanapatiwa ushauri wa awali, huku baadhi ya kesi au malalamiko yanayoihitaji mamlaka nyingine yakielekezwa kwenye taasisi zenye jukumu la kuyashughulikia.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya sheria na kufahamu wapi pa kupeleka changamoto zao. Masuala mengi yanayowasilishwa ni ya mirathi, ardhi na jinai, hivyo tunawashauri na kuwaelekeza kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kupata suluhu,” amesema.
Wizara hiyo imewataka wananchi kuendelea kujitokeza katika siku zilizobaki za maonesho hayo, ili kutumia huduma zinazotolewa na kupata msaada wa kisheria unaoweza kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika jamii.
Ushiriki wa Wizara ya Katiba na Sheria katika Sabasaba unaendelea kuwa daraja muhimu la kuwafikishia wananchi huduma za haki na sheria kwa karibu, sambamba na kuimarisha uelewa wao kuhusu wajibu na stahiki zao kisheria.




