DODOMA YAJENGA SEKTA BINAFSI KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2050

 


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuendelea kuijenga na kuilea sekta binafsi, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za ajira na kuharakisha maendeleo ya wananchi.


Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, alipotembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Alhaj Shekimweri amesema ushiriki wa jiji hilo katika maonesho hayo pamoja na kuwapa nafasi wajasiriamali wa sekta binafsi kuonesha bidhaa zao ni uthibitisho wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Baraza la Biashara Wilaya ya Dodoma.


Amesema sekta binafsi ni injini muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Dodoma na taifa kwa ujumla, hivyo ushirikishwaji wake ni nguzo ya kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


“Nimefurahi kuona siyo wataalam wa jiji pekee waliokuja, bali pia mmeshakuja na wajasiriamali wa sekta binafsi. Hii inaonesha mmeielewa dira tuliyonayo katika wilaya na mkoa wetu ya kujenga uwezo wa wajasiriamali kufanya biashara za kimataifa,” amesema.



Ameeleza kuwa mwezi Aprili mwaka huu, Baraza la Biashara Wilaya ya Dodoma lilifanya ziara ya mafunzo jijini Dar es Salaam, ambapo walitembelea Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu ya Kwala kwa lengo la kujifunza namna ya kuwaandaa wafanyabiashara wa Dodoma kushiriki kikamilifu katika biashara za kimataifa.


Kwa mujibu wa Alhaj Shekimweri, tathmini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeonesha kuwa takribani asilimia 70 ya utekelezaji wake inategemea mchango wa sekta binafsi.


“Hatuwezi kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bila kushirikisha sekta binafsi. Hivyo, hatua ya Jiji la Dodoma kuwaleta wajasiriamali kwenye maonesho haya ni jambo la kupongezwa na kuigwa,” amesema.


Katika ziara yake, Alhaj Shekimweri alivutiwa na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali, hususan viungo vinavyotengenezwa na Furahia Food Spices, vikiwemo masala ya chai, pilau na nyama.


Amesema bidhaa hizo zinaonesha kiwango kikubwa cha maarifa, ubunifu na uwezo wa wajasiriamali wa Dodoma kuzalisha bidhaa zenye ushindani sokoni.


“Nimeona viungo vya aina mbalimbali na ubunifu mkubwa unaoletwa sokoni. Niwapongeze sana Jiji la Dodoma kwa ushiriki wenu, kwa kweli nimefarijika sana kuwaona hapa,” amesema.




🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post