Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wanakabiliwa na changamoto ya kukosa chakula kutokana na kutelekezwa na familia zao wakati wakiendelea kupatiwa matibabu.
Kutokana na hali hiyo, wadau wa masuala ya kijamii wamejitokeza kutoa msaada wa chakula kwa wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya katika hospitali hiyo, ikiwa ni sehemu ya kusaidia makundi yenye uhitaji mkubwa.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa chakula hospitalini hapo, mmoja wa viongozi wa Shamsia Women Group, Hidaya Rusheke, alisema lengo la msaada huo ni kuwasaidia wagonjwa wanaoshindwa kupata chakula kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo umaskini na kutokuwa na ndugu wa kuwahudumia.
“Wapo wagonjwa ambao wanashindwa hata kupata mlo mmoja wakiwa hospitalini. Wengine hawana familia kabisa, huku wengine wakitelekezwa na ndugu zao. Mgonjwa hawezi kutumia dawa vizuri bila kupata chakula,” alisema Rusheke.
Alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jai imeona umuhimu wa kutoa msaada huo si kwa wagonjwa pekee bali pia kwa wahudumu wa afya, hasa kipindi hiki cha sikukuu ambapo baadhi ya huduma muhimu huwa zimefungwa.
Rusheke pia alitoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kutembelea na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu waliolazwa hospitalini pamoja na kujitolea michango mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia.
Kwa upande wake, Mratibu wa Jai, Abdilah Magomba, alisema taasisi hiyo hupokea zaidi ya watu 200 wenye mahitaji mbalimbali kila mwaka, ikiwemo chakula, gharama za matibabu na misaada mingine ya kibinadamu.
Alisema ongezeko la watu wenye uhitaji limewasukuma kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wagonjwa na makundi mengine yenye changamoto wanapata msaada unaostahili.
Naye mmoja wa wagonjwa waliopokea msaada huo, Florenciana Sogole, aliwashukuru wadau hao kwa msaada walioutoa akisema umewapa faraja kubwa wakati wa matibabu yao hospitalini.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.






