Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Wanawake kutoka maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kukutana katika kongamano kubwa la kiroho litakalofanyika kuanzia Juni 9 hadi 12, 2026 katika ofisi za Makao Makuu ya KEPT zilizopo Ihumwa jijini Dodoma, likiwa na lengo la kuombea Taifa, vijana, watoto pamoja na kuimarisha maadili ya jamii.
Kongamano hilo litakaloanza saa 3:00 asubuhi kila siku, limeelezwa kuwa ni mkusanyiko maalumu wa wajenzi wa mwili wa Kristo, hasa wanawake waombolezaji wenye wito wa kusimama mbele za Mungu kwa maombi ya toba na rehema kwa ajili ya Taifa.
Waandaaji wa kongamano hilo wamesema dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali za mmomonyoko wa maadili ikiwemo ongezeko la vitendo vya ukatili, mauaji, ushoga na ulawiti, hali inayohitaji maombi ya dhati na toba mbele za Mungu.
Wamefafanua kuwa ujumbe wa kongamano hilo umejengwa katika maandiko ya WARUMI 1:22-27 pamoja na YEREMIA 9:17-21 yanayosisitiza mwito wa wanawake waombolezaji kusimama na kulilia Taifa ili Mungu aondoe ghadhabu yake na kuleta uponyaji kwa jamii.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Askofu wa Kanisa la Elim Pentekoste Tanzania Jimbo la Dodoma, Askofu Zephania Bahe, huku wachungaji na viongozi mbalimbali wa kiroho wakitarajiwa kushiriki.
Miongoni mwa viongozi watakaohudhuria ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanawake Elimu Pentekoste Tanzania (IWEPT), Askofu Furaha Simtenda pamoja na Mkurugenzi wa IWEPT Jimbo la Dodoma, Glory Ibrahim.
Waandaaji wameeleza kuwa kongamano hilo litakuwa siku tatu za “Kambi la Baraka” kwa kila mwanamke, likiwa na vipindi vya maombi, mafundisho ya kiroho, maombezi pamoja na nyakati za ibada.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni: “MWANAMKE MWEMA NI NGUZO YA NYUMBA NA BARAKA KWA JAMII,” ikitokana na maandiko ya Mithali 31:10-31.
Kwa mawasiliano na ushiriki zaidi, wananchi wametakiwa kuwasiliana kupitia namba 0682411135.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

