SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI, YALENGA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA WATOTO WACHANGA

 


Na, Wellu Mtaki, Dodoma 📍


Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya afya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya vyenye vyumba vya upasuaji ili kusogeza huduma karibu na wananchi.



Amesema hayo  Naibu Waziri wa Afya Dkt.  Florence Samizi kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Kongamano la nne la Kisayansi la Chama cha Wataalam wa Dawa za Usingizi na Ganzi Tanzania.



Amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za dawa za usingizi tiba na ganzi salama ili kuboresha usalama wa upasuaji na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini.



Dkt. Samizi amesema wataalamu hao ni muhimili muhimu katika kuhakikisha huduma salama za upasuaji zinapatikana nchini.




Pia amewapongeza wataalamu wa usingizi na ganzi kwa mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma za afya, akibainisha kuwa taaluma hiyo ina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha upasuaji unafanyika kwa usalama na ufanisi.


Amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto zinazoikabili taaluma hiyo pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha huduma, hususan katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.


Aidha, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mafunzo ya taaluma hiyo kwa kuimarisha vyuo vinavyotoa kozi za usingizi na ganzi kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu.




Sambamba  na hayo ameeleza kuwa kuwa Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya afya ili kuimarisha utoaji wa huduma na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali muhimu, huku ikiendelea kutafuta vyanzo vya mapato ili kuendeleza sekta hiyo.

Previous Post Next Post