Programu ya Urasimishaji Ujuzi Kuwafikia Walengwa Bila Ubaguzi


Na Wellu Mtaki - DODOMA.📍


 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, ameiagiza VETA kuhakikisha Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi inawafikia walengwa wote bila ubaguzi.


Akizindua programu hiyo jijini Dodoma Aprili 22, 2026, Prof. Mkenda amesema amesema programu hiyo inaendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na marejeo ya 2023.


Aliwataka waajiri kushirikiana na vijana watakaonufaika na mpango huo unaotekelezwa na VETA kwakuwa wametambuliwa kuwa wana ujuzi wa kutosha wa kufanya kazi kwa ufanisi.


Alisema programu hiyo inafadhiliwa na serikali kwa asilimia 100 hivyo wanufaika hawatalipia gharama yoyote kwani unaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaolenga kuimarisha rasilimali watu na kuongeza ushindani wa uchumi wa viwanda.


Naibu Waziri wa Elimu, Wanu Hafidhi Amir, alisema programu hiyo itawapa vijana sifa ya kushindana kikamilifu katika soko la ajira ndani na nje ya nchi. 


Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Antony Kasore, alisema wanufaika 14,400 wanatarajiwa kushiriki katika awamu ya kwanza ya utekelezaji huku jumla ya washirika wote ikitarajiwa kufikia vijana 30,000.


Baadhi ya wanufaika walisema mpango huo utawasaidia kupata ajira na fursa za zabuni kutokana na ujuzi wao kutambuliwa rasmi.

Previous Post Next Post