WASANII WAASWA KUCHANGAMKIA MIKOPO HADI MILIONI 100 KUTOKA MFUKO WA UTAMADUNI




Na Mwandishi Wetu, Dodoma📍


Wasanii zaidi ya 35 wa kwaya ya WASANI Choir inayopatikana Chamae, wilayani Kongwa mkoani Dodoma wamepatiwa mafunzo ya uongozi, usimamizi wa fedha pamoja na namna ya kupata mikopo kupitia Mfuko wa Sanaa na Utamaduni Tanzania.


Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewa na mkufunzi wa masuala ya uongozi, sanaa na usimamizi wa fedha, CFE Naamala Samson, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha sanaa na utamaduni cha Chamwino Arts Centre (CAC) kilichopo Chamwino Ikulu, Dodoma.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Naamala aliwahimiza wasanii nchini kutambua na kuchangamkia fursa zilizopo kupitia Mfuko wa Sanaa na Utamaduni, akieleza kuwa wasanii wanaweza kupata mikopo kuanzia shilingi laki mbili hadi shilingi milioni 100.



“Natoa wito kwa wasanii kutambua kuwa tuna fursa kubwa ya kupata mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni kuanzia shilingi laki mbili hadi shilingi milioni mia moja,” alisema Naamala.


Alieleza kuwa lengo la mfuko huo ni kuinua ubora wa kazi za sanaa na utamaduni ili ziweze kujiendesha kibiashara, kuzalisha ajira pamoja na kuchangia katika pato la taifa.


Kwa nyakati tofauti, viongozi, walezi pamoja na wanakwaya wa WASANI Choir walimshukuru mkufunzi huyo kwa mafunzo hayo wakisema yamewaongezea maarifa kuhusu namna bora ya kusimamia kwaya yao pamoja na kubuni miradi ya kiuchumi.


Walieleza kuwa kupitia elimu hiyo wataweza kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo na kukamilisha taratibu zinazohitajika ili kupata mikopo kutoka Mfuko wa Sanaa na Utamaduni kwa lengo la 

kuongeza vifaa vya kwaya yao na kujiongezea kipato.


Mfuko wa Sanaa na Utamaduni umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ujumuisho wa Wadhamini (Trustees’ Incorporation Act) ya mwaka 2002 (CAP. 318 R.E. 2002) na kupewa hati ya usajili namba 1776 tarehe 30 Septemba, 2020.


Mfuko huo unalenga kuwasaidia wasanii wa sekta mbalimbali ikiwemo muziki, filamu, maonesho ya sanaa pamoja na ufundi ili kukuza na kuendeleza sekta ya sanaa na utamaduni nchini.





🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post