Na Carlos Claudio, Dodoma📍
Wananchi wa Kata ya Tambukareli jijini Dodoma wamepongezwa kwa mshikamano na ushirikiano wanaouonyesha katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Pongezi hizo zimetolewa na Diwani wa Kata ya Tambukareli, Mhe. Clinton Manzi, wakati akizungumza na wananchi katika hafla ya futari aliyoiandaa kwa wakazi wa kata hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Msikiti wa Masjid Latif jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Manzi aliwashukuru wananchi kwa kuitikia mwaliko wake na kujitokeza kwa wingi kushiriki futari hiyo, akieleza kuwa ushirikiano wao unawatia moyo vijana wanaojitokeza kuongoza na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii.
“Niwapongeze sana wananchi wangu wa Tambukareli kwa ushirikiano wenu. Nawashukuru kwa kuitikia mialiko hii. Mimi napenda sana kuona namna mnavyotutia moyo sisi vijana wenu,” amesema Mhe. Manzi.
Aliongeza kuwa anathamini sana jitihada za wananchi waliojitokeza katika hafla hiyo, akibainisha kuwa baadhi yao walitoka mbali na kuacha shughuli zao za kila siku ili kushiriki tukio hilo muhimu la kijamii.
“Niwakaribishe sana na Mwenyezi Mungu awabariki kwa pale mlipopungukiwa. Najua wengine mmetoka mbali na kuacha shughuli zenu na kusema leo mje kufuturu kwa kijana wenu,” aliongeza.
Hafla hiyo ya futari ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa kutoka maeneo tofauti ya jijini Dodoma.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Silas Makanyaga, aliyemwakilisha Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema mbunge huyo alishindwa kuhudhuria kutokana na majukumu mengine ya kikazi na hivyo kumtuma yeye kumwakilisha.
“Nawapongeza wananchi wote pamoja na viongozi waliotumia muda wao kufika hapa. Ushirikiano unatokana na watu, na watu ndiyo sisi,” alisema Makanyaga.
Aidha alimpongeza Mhe. Manzi kwa kuandaa futari hiyo akisema ni jambo jema hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Ninampongeza kwa dhati diwani wetu wa Kata ya Tambukareli kwa kufanya jambo hili la kheri. Tunaomba Mungu azidi kumsaidia kwa kuwa wakati aliouchagua kufanya matendo ya huruma ni sahihi,” aliongeza.
Naye Diwani wa Kata ya Makole, Mhe. Omari Omari, akizungumza kwa niaba ya madiwani wa Jiji la Dodoma, alimpongeza Mhe. Manzi kwa kuonesha upendo wa dhati kwa wananchi wake.
“Sisi tunakushukuru sana na kukupongeza kwa upendo wako juu ya wananchi wa Tambukareli. Umefanya jambo jema sana hasa katika mwezi huu wa Ramadhani na Kwaresma kwa kuwafuturisha watu. Mwenyezi Mungu akujalie kheri,” alisema.
Kwa upande wake Polisi Kata wa Tambukareli, Inspekta Neema Seme, alimpongeza Mhe. Manzi kwa ushirikiano anaouonyesha katika kata hiyo, hususan kwa vijana.
Alisema diwani huyo amekuwa karibu na vijana kwa kuwasikiliza na kushirikiana nao kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Tuna bahati kuwa na diwani kijana anayeelewa changamoto za vijana wenzake na kushirikiana nao katika kutafuta suluhisho kwa manufaa ya wananchi wa Tambukareli,” alisema Inspekta Seme.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni madiwani kutoka kata mbalimbali ikiwemo Makulu, Makole na Chidachi, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Dodoma Mjini, Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Dodoma Mjini, wenyeviti wa mitaa, watendaji wa serikali za mitaa pamoja na viongozi wa dini.
Futari hiyo imelenga kuimarisha mshikamano, upendo na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kipindi hiki cha Kwaresma na mwezi mtukufu wa Ramadhani.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)