DIWANI JENESTA MALINGO KUANZA ZIARA YA SIKU TATU KATA YA ZUZU


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Diwani wa Kata ya Zuzu, Mhe. Jenesta Malingo, anatarajiwa kuanza ziara ya siku tatu katika mitaa mitano ya kata hiyo kuanzia Machi 17 hadi Machi 19, 2026, kwa lengo la kukutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.


Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Mhe. Malingo ataanza ziara yake siku ya Jumanne Machi 17, 2026 ambapo atatembelea mitaa ya Chididimo na Sokoine kuanzia saa 9:30 hadi 11:00 jioni, akikutana na wananchi na viongozi wa mitaa hiyo.


Siku ya Jumatano Machi 18, 2026 ziara itaendelea katika Mtaa wa Pinda kuanzia saa 9:30 hadi 13:00 mchana, kisha kuendelea katika Mtaa wa Mazengo kuanzia saa 13:10 hadi 15:30 mchana ambapo wananchi watapata fursa ya kuwasilisha changamoto zao pamoja na kupokea maelezo kuhusu maendeleo yanayotekelezwa katika kata hiyo.


Ziara hiyo itahitimishwa siku ya Alhamisi Machi 19, 2026 katika Mtaa wa Soweto kuanzia saa 10:30 hadi 15:00 mchana.


Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Mhe. Malingo amesema kuwa pamoja na kukutana na wananchi, pia atatumia fursa hiyo kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ambapo chama hicho kilipata ushindi mkubwa.


Aidha, ziara hiyo itatoa nafasi ya kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya kata, kueleza hatua za utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya Kata ya Zuzu pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.


Pia, diwani huyo atahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shuleni kabla ya Machi 31, 2026 ili kuendelea na masomo yao bila kukosa haki yao ya elimu.


Wananchi wa Kata ya Zuzu wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo ili kushiriki katika mijadala ya maendeleo ya kata yao na kutoa maoni yatakayosaidia kuimarisha ustawi wa jamii.

“KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE.”


🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post