CHAKUHAWATA YATAJA CHANGAMOTO ZA WALIMU, YAOMBA USHIRIKIANO ZAIDI KWA WAJIR

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mwenyekiti wa Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (CHAKUHAWATA), Emmanuel Herman, amesema licha ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa chama hicho, bado walimu wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha ustawi wa wanachama wake.


Akizungumza Machi 14, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha viongozi wa chama kutoka wilaya mbalimbali za Tanzania Bara, Herman ameeleza kuwa baadhi ya waajiri bado hawatoi ushirikiano unaohitajika kwa chama hicho.


Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kutokutekeleza ipasavyo makato ya ada za wanachama waliojiunga na chama hicho, licha ya walimu hao kukamilisha taratibu zote za uanachama.


“Licha ya mfanyakazi kuwa na haki ya kisheria ya kujiunga au kuhama chama cha wafanyakazi, bado kuna baadhi ya waajiri hawatekelezi wajibu wao wa kuingiza makato ya ada za wanachama wetu,” alisema Herman.



Aidha, alibainisha kuwa chama hicho pia hakishirikishwi kikamilifu katika mabaraza ya wafanyakazi yanayofanyika katika halmashauri mbalimbali, hali inayowanyima wanachama wake uwakilishi katika majadiliano yanayohusu maslahi yao.


Changamoto nyingine aliyoitaja ni baadhi ya walimu viongozi wa chama kuhamishwa kutoka maeneo yao ya kazi bila sababu za msingi na wakati mwingine bila kupewa stahiki zao za uhamisho. 


Kwa mujibu wa Herman, hatua hizo zimekuwa zikidhoofisha maendeleo ya chama na kuwakatisha tamaa walimu wengine wanaotaka kujiunga nacho.


Pia alieleza kuwa kuna matukio ya waajiri kuingiza makato ya ada za vyama viwili vya wafanyakazi kwa wakati mmoja katika mishahara ya baadhi ya wanachama, jambo alilosema ni kinyume na taratibu na sheria za kazi.


Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo alilalamikia baadhi ya wanachama wa CHAKUHAWATA kutoshirikishwa katika maadhimisho ya International Workers' Day (Mei Mosi), huku wakati mwingine wakiondolewa katika maandamano wanapojitokeza kushiriki pamoja na wafanyakazi wa vyama vingine katika baadhi ya mikoa nchini.


Licha ya changamoto hizo, Herman alisema chama hicho kimepiga hatua kubwa tangu kilipoanzishwa mwaka 2015 katika mkoa wa Kigoma kikiwa na wanachama 182 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji.



Alisema hadi kufikia Februari 2026, idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia 49,750 nchi nzima, huku zaidi ya walimu 3,000 wakiwa wameomba kujiunga na chama hicho.


Kwa mujibu wa Herman, chama hicho pia kimefanikiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wa matawi na wilaya katika wilaya 84 na kinatarajia kufanya uchaguzi katika wilaya 44 zilizotimiza masharti ya kikatiba.


Aliongeza kuwa CHAKUHAWATA kimeweza kujenga mahusiano mazuri miongoni mwa walimu na kuimarisha ushirikiano na serikali kwa kutatua changamoto kwa njia ya mazungumzo.


Mbali na hilo, chama hicho kimeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wanachama wake ikiwemo kusaidia walimu wanaokumbwa na matatizo ya kiafya, kesi za kikazi, majanga ya moto na kusaidia wastaafu pamoja na shughuli nyingine za kijamii.


Vilevile, chama kimekuwa kikisaidia taasisi za elimu kwa kutoa vifaa kama mashine za kufanyia nakala, kompyuta pamoja na vifaa vya ujenzi kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari nchini.


Katika hatua ya kuboresha uendeshaji wa shughuli zake, Herman alisema Mkutano Mkuu wa chama uliofanyika Januari 2025 ulipitisha azimio la kuhamisha makao makuu ya chama kutoka Kigoma kwenda Dodoma ili kurahisisha shughuli za chama kutokana na mji huo kuwa makao makuu ya nchi.


Alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kufuatilia haki na stahiki za wanachama wake pamoja na kuhakikisha walimu wanatekeleza majukumu yao kikamilifu katika maeneo yao ya kazi.




🚨FULL Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post