SERIKALI YAIMARISHA MAFUNZO YA UANAGENZI, YATENGA BILIONI 4.3 KUWAINUA VIJANA NA WENYE MAHITAJI MAALUM


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma.

 Serikali imezitaka taasisi na vyuo vinavyotekeleza mafunzo ya uanagenzi nchini kuhakikisha vinatoa fursa sawa kwa vijana wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, ili kuwawezesha kujitegemea na kuondoa dhana potofu kuwa ni tegemezi katika jamii.


Rai hiyo imetolewa leo Machi3,2026  jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mafunzo ya Uanagenzi Awamu ya Nane kwa mwaka 2025/2026, yenye kaulimbiu isemayo “Nguvu Kazi yenye Ujuzi Stahili kwa Ajira Endelevu.”


Mhe. Sangu amesisitiza kuwa vyuo vilivyopata nafasi ya kushiriki katika programu hiyo vinapaswa kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira ili wahitimu wanapotoka wawe na uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi.



“Tuendelee kuhakikisha vijana wanapata mafunzo stahiki ili wanapotoka hapa wadhihirishe kuwa wana uwezo na si tegemezi. Lazima muendane na teknolojia ya kazi akili unde (Artificial Intelligence); si jambo la baadaye tena. Maarifa ya kisasa ni lazima,” amesema.


Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka msisitizo katika kukuza ajira kwa vijana, akieleza kuwa uwekezaji wa shilingi bilioni 4.3 umetengwa ili kuimarisha na kupanua programu hiyo. Ameongeza kuwa serikali ina mpango wa kuongeza bajeti zaidi ili vijana wengi wanufaike.


“Siyo vijana wote wamepata fursa hii. Thaminini nafasi mliyopewa, mkafanikiwe, mjiajiri na kuajiri wengine,” amesisitiza.


Amebainisha kuwa ukosefu wa ajira unatokana kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa ujuzi miongoni mwa vijana, hivyo serikali imeamua kuimarisha programu za kukuza ujuzi ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga taifa la ubunifu na lenye ushindani.



Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Zuhura Yunus, aliyemwakilisha Katibu Mkuu, amesema lengo la uzinduzi huo ni kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika mafunzo ya uanagenzi, kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, pamoja na kusisitiza umuhimu wa ujuzi katika kukuza ajira na uchumi wa taifa.


Ameeleza kuwa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ilianza kutekelezwa mwaka 2016/2017 kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma. Hadi kufikia Februari mwaka huu, jumla ya wanufaika 168,657 wamepata mafunzo kupitia programu hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema mkoa huo umejipanga kutekeleza kikamilifu maelekezo ya serikali, ikiwemo kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya kuwawezesha vijana. 


Amesema Dodoma ina fursa nyingi za ajira na kujiajiri, lakini vijana wanapaswa kuwa na dhamira, bidii na utayari wa kuzitumia.



Akizungumzia changamoto ya miundombinu, hasa barabara zinazoelekea kwenye baadhi ya vyuo, ameahidi kushirikiana na TARURA ili kuingiza maboresho hayo katika bajeti ijayo ya mwezi Julai.


Naye Mwakilishi wa Waajiri, Bw. Joseph Kimweri, amesema waajiri wana imani na uwezo wa vijana wanaopata mafunzo hayo, lakini amewataka kuzingatia maadili na kuwa na udadisi katika kazi zao.

“Ulimwengu wa ukarimu unabadilika. Tuwe wataalamu wenye maadili na tusipoteze mguso wa kibinadamu unaofafanua tasnia hii,” amesema.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Don Bosco, Bw. Justine Mulega, amesema chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1982, kinatoa mafunzo kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya sita na kwa sasa kina wanagenzi 235, wakiwemo wasichana 74 na wavulana 161.


Ameiomba serikali kuendelea kusaidia upatikanaji wa vifaa na nyenzo za kufundishia ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu, pamoja na kuboresha barabara inayoelekea chuoni hapo ambayo huwa haipitiki wakati wa masika.


Hafla hiyo imeonesha dhamira ya serikali ya kuendelea kuwekeza katika ujuzi kama nguzo muhimu ya ajira endelevu na maendeleo ya taifa.







🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.
Previous Post Next Post