Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya inaendesha kikao kazi cha kuandaa zana za kufanyia Tathmini ya Ubora wa Takwimu (Data Quality Assessment – DQA) za ufuatiliaji wa magonjwa, hali na matukio yenye athari kiafya nchini. Kikao hicho kinafanyika mkoani Morogoro, kikikusanya wataalamu wa afya na takwimu kutoka ngazi mbalimbali.
Kazi hii inatekelezwa kupitia mradi wa Pandemic Fund, unaoratibiwa na Amref Health Africa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya. Mradi huo unalenga kuimarisha maandalizi na mwitikio dhidi ya milipuko ya magonjwa pamoja na majanga ya kiafya.
Kupitia zana hizi za DQA, timu za wataalamu zitawezesha zoezi la kuhakiki ubora wa takwimu katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
Tathmini hiyo itazingatia viashiria muhimu kama usahihi wa takwimu, ukamilifu wa taarifa, uwasilishaji kwa wakati na ulinganifu wa taarifa kutoka ngazi ya vituo vya kutolea huduma hadi taifa.
Lengo kuu la kikao kazi hiki ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na takwimu bora za ufuatiliaji wa magonjwa zitakazosaidia:
Kutambua viashiria vya milipuko mapema.
Kuchukua hatua za tahadhari kwa wakati.
Kupanga rasilimali kwa ufanisi.
Kudhibiti na kupunguza athari za milipuko kwa jamii.
Kwa kuimarisha ubora wa takwimu, Tanzania itaongeza uwezo wake wa kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi na hivyo kuimarisha usalama wa afya ya umma kwa ujumla.




