WIZARA YA ARDHI YAANZISHA ‘SAMIA ARDHI KLINIKI’ KUONGEZA UMILIKI WA ARDHI KWA WANAWAKE


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha kliniki maalum iitwayo Samia Ardhi Kliniki nchi nzima kwa lengo la kuongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi, ambapo kwa sasa ni asilimia 28 pekee.


Hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha huduma za ardhi zinatolewa kwa kuzingatia misingi ya usawa wa kijinsia.


Akizungumza Machi 2, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, amesema mpango huo utaendeshwa nchi nzima na unatarajiwa kuhitimishwa Machi 7 mwaka huu, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.


Amesema lengo kuu la Samia Ardhi Kliniki ni kuongeza asilimia ya umiliki wa ardhi kwa wanawake kupitia utoaji wa elimu, hati za umiliki na utatuzi wa migogoro ya ardhi.


“Takwimu zinaonesha kuwa ni takriban asilimia 28 pekee ya wanawake nchini wanamiliki ardhi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha ushiriki wao katika masuala ya umilikishaji,” amesema Mhandisi Sanga.


Amefafanua kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 iliweka msingi wa usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi kati ya wanaume na wanawake, lakini changamoto zilijitokeza katika utekelezaji, hususan kwenye masuala ya mirathi na urithi ambako mila na desturi zilichangia kuwabagua wanawake.


“Tamko la sera ya mwaka 1995 lilielekeza kuzingatia mila na desturi, lakini katika Sera mpya ya mwaka 2025 iliyozinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, haki ya umiliki wa ardhi kwa wanaume na wanawake imewekewa usawa bayana,” amesema.


Ameongeza kuwa katika sera hiyo mpya, masuala ya urithi na mirathi yameainishwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, hivyo kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kumiliki na kurithi ardhi bila ubaguzi.


Kupitia kliniki hiyo maalum, wanawake wanapatiwa hati za umiliki wa ardhi, kusaidiwa kutatua migogoro pamoja na kupewa elimu kuhusu haki na taratibu za umiliki wa ardhi.


Mpango huo unalenga kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta ya ardhi zinatatuliwa kwa wakati, huku ukichochea ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla. 


Mhandisi Sanga amewataka wananchi kuwa watulivu wakati zoezi hilo likiendelea ili waweze kuhudumiwa kwa weledi.


Kwa upande wake, Mthamini Mkuu wa Serikali kutoka wizara hiyo, Bi. Evelyn Baruti Mugasha, amesema hadi majira ya mchana wanawake zaidi ya 160 walikuwa wamejitokeza kupata hati, huku wengine wakiendelea kujitokeza.


Bi. Mugasha amewahimiza wanawake wa Mkoa wa Dodoma kutumia fursa hiyo kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali, huku akitoa wito kwa wanaume kutoa ushirikiano ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika umiliki wa ardhi.


“Kumwezesha mwanamke kumiliki ardhi ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa familia na taifa kwa ujumla,” amesema.


Wananchi wa Mkoa wa Dodoma wamempongeza Rais Samia kwa kuwapa kipaumbele wanawake katika suala la umilikishaji wa hati ili kuhakikisha hawabaki nyuma.


Mkazi wa Chidachi, Bi. Veronica Hamisi, amesema amefurahi kupata hati aliyokuwa akiifuatilia kwa takribani miaka mitatu ndani ya siku moja.


Kwa upande wake, mkazi wa Miyuji, Getruda Mathias, amesema amehangaika kwa miaka mitano kupata hati, lakini kupitia kliniki hiyo ameweza kuipata ndani ya saa moja bila usumbufu.


“Nawasihi wanawake wenzangu tujitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii ambayo itahitimishwa Machi 7 mwaka huu,” amesema.


Naye mkazi wa Ilazo, Zena Hamis, amemshukuru Rais kwa kuwapa kipaumbele wanawake na kuwasihi ambao bado hawajajitokeza kufanya hivyo ili kunufaika na huduma hiyo muhimu.





🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.
Previous Post Next Post