Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeandaa kikao kazi cha kuandaa “Standardise Addendum” ya moduli za ufuatiliaji wa magonjwa yaliyopewa kipaumbele kwa ajili ya kutumika katika mitaala ya vyuo vya afya kada za kati na wahudumu wa afya ngazi ya jamii nchini.
Kikao hicho kinafanyika Mkoani Morogoro kikilenga kuboresha na kuhuisha maudhui ya mitaala ya mafunzo ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi sahihi wa kutambua, kufuatilia na kutoa taarifa za magonjwa yaliyopewa kipaumbele.
Hatua hiyo inafuatia mapitio yaliyofanywa na Wizara kubaini mapungufu katika baadhi ya maudhui ya ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za magonjwa hayo kwenye mitaala ya vyuo vya afya na Sayansi Shirikishi kwa kada za kati pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Kupitia kikao hiki, Wizara inalenga kuimarisha ubora wa mafunzo, kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa magonjwa na kuhakikisha taarifa za afya zinakusanywa na kuripotiwa kwa usahihi, hatua itakayochangia katika kuboresha huduma za afya na kufikia malengo ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa.



