📌Aweka bayana Dhamira ya Serikali ni Kupunguza Magonjwa Yasiyoambukiza.
Mkurugenzi wa Huduma za Uhamasishaji wa Afya katika Wizara ya Afya Tanzania, Dkt. Rahma Ahmed Hingora, amehimiza watumishi wa Elimu ya Afya kwa Umma kufanya kazi kwa ushirikiano, kujituma na uwajibikaji ili kuimarisha utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi.
Dkt. Hingora ametoa wito huo wakati alipokutana na watumishi wa Idara hiyo katika kikao kilichofanyika Dodoma, ambapo alisisitiza kuwa mafanikio ya programu za uhamasishaji wa afya yanategemea mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi.
Halikadhalika amesema dhamira ya Serikali ni kupunguza Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD's).
"Kupitia Elimu ya afya kwa umma dhamira yetu kubwa ni kupunguza kasi ya NCD’s na kupunguza kasi ya magonjwa ya kuambukiza ili kuimarisha Jamii yenye afya bora na kuongeza nguvu kazi, kwa kuimarisha Jamii yenye afya bora tutakuwa tumepunguza msongamano kwenye hospitali zetu"amesema.
Amesema Elimu ya Afya kwa Umma ina jukumu muhimu la kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa, kuzingatia usafi wa mazingira, lishe bora pamoja na kuishi maisha yenye afya.
“Ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana katika kutekeleza majukumu yetu, kwani kwa kufanya hivyo tutaweza kufikisha ujumbe wa afya kwa wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Dkt. Hingora.
Aidha, amewahimiza watumishi hao kuendelea kujituma katika majukumu yao na kutumia ubunifu katika kuandaa na kusambaza ujumbe wa elimu ya afya kwa makundi mbalimbali ya jamii.
Kwa upande wao, watumishi wa Elimu ya Afya kwa Umma wameeleza utayari wao wa kuendeleza ushirikiano na kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha elimu ya afya inawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.








