Na Jasmine Shamwepu, Dodoma📍
Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeanza utekelezaji wa tafiti mbalimbali zenye lengo la kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na isiyo rasmi pamoja na uzalishaji wa viwanda nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Sensa na Tafiti za Kijamii wa NBS, Dkt. Amina Msengwa, amesema tafiti hizo zinalenga kupata takwimu sahihi kuhusu uzalishaji, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara ili kubaini mwenendo wa ukuaji wa biashara na viwanda nchini.
Amesema taarifa zitakazokusanywa kupitia tafiti hizo zitaisaidia Serikali pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti kubuni programu na mikakati madhubuti ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kwa mujibu wa Dkt. Msengwa, utafiti huo pia utahusisha ukusanyaji wa taarifa kuhusu uzalishaji viwandani, ikiwemo orodha ya viwanda vilivyopo katika mikoa mbalimbali, aina ya bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi, gharama za uzalishaji pamoja na mapato yanayopatikana viwandani.
Ameongeza kuwa tafiti hizo zitafanyika katika maeneo 1,518 ya utafiti nchini ambapo biashara na taasisi 8,624 pamoja na viwanda 4,245 vinatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.
Serikali imewataka wananchi watakaofikiwa na wadadisi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu bora zitakazosaidia kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa kwa ufanisi.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA



