UMEME WA UHAKIKA DODOMA NA IRINGA: KITUO CHA KUPOOZA UMEME MTERA CHAZINDULIWA


Na Carlos Claudio, Iringa.📍


Wizara ya Nishati imeridhia na kuanza kutekeleza kikamilifu Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha umeme unapelekwa katika vijiji vyote vilivyosalia nchini ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.


Akizungumza leo Januari 16, 2026 mkoani Iringa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Mtera, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratias Ndejembi, amesema hakuna kijiji wala kitongoji kitakachoachwa katika mpango huo wa serikali wa kusambaza umeme nchi nzima.


Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuijenga Tanzania kuwa na uchumi wa kisasa, unaokua kwa kasi na wenye ushindani.


“Bwawa la Mtera lilianza kuzalisha umeme mwaka 1980 kwa megawati 80, lakini kwa zaidi ya miaka 40 hakukuwa na uwekezaji mkubwa kama huu tunaouona leo. Huu ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Waziri Ndejembi.


Waziri huyo amesema kituo hicho kimejengwa mahsusi kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme katika wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma pamoja na wilaya ya Kilolo na maeneo ya Isimani mkoani Iringa, ambako kwa miaka mingi wawekezaji walikwamishwa na tatizo la umeme mdogo (low voltage).




Kwa mujibu wa Waziri, hali ya awali iliwalazimu wamiliki wa viwanda vidogo kama mashine za kusaga na kukamua mafuta kufanya kazi nyakati za usiku pekee, jambo lililopunguza uzalishaji na kukatisha tamaa wawekezaji.


“Leo hii mwekezaji anaweza kuwekeza bila hofu. Umeme wa uhakika unapatikana mchana na usiku, viwanda vinafanya kazi kikamilifu, ajira zinaongezeka na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unakua,” alisisitiza.


Ameongeza kuwa sekta ya nishati, hususan umeme, ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama, nafuu na endelevu kwa Watanzania wote.


Upanuzi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Mtera umeimarisha miundombinu ya umeme, hususan kwa maeneo ya vijijini na yale yenye fursa kubwa za kiuchumi, hivyo kuweka msingi imara wa maendeleo ya viwanda, biashara na ujasiriamali.




Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said, amesema mradi unalenga kusambaza umeme katika vijiji 121 ambavyo havikunufaika na mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga.


Ameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa kituo hicho, umeme ulikuwa ukisafirishwa kwa zaidi ya kilomita 155 kutoka Kituo cha Zuzu, hali iliyosababisha upotevu mkubwa wa umeme na kukatika mara kwa mara.


“Mradi umehusisha ujenzi wa transfoma mbili za kupunguza umeme kutoka kilovolti 220 hadi 33 kwa ajili ya usambazaji. Kituo kina njia nne za kusambaza umeme, ambapo mbili ni za msongo wa kati wa kilovolti 33 zenye uwezo wa kupitisha hadi megawati 14 kila moja kwa mikoa ya Dodoma na Iringa,” amesema.


Ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa asilimia 100 na tayari kinafanya kazi, ambapo kwa sasa Dodoma inapokea megawati sita na Iringa megawati tatu, huku mahitaji yakiongezeka kutokana na wawekezaji wanaojitokeza kufungua viwanda na migodi.


Mradi huo umegharimu Shilingi bilioni 9.7, ambapo asilimia 50 ya fedha zilitolewa na Serikali ya Sweden na asilimia 50 na Serikali ya Norway. Serikali imewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya nishati nchini.


Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Simon Songe, amewasisitiza wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya umeme ili miradi hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa manufaa yaliyokusudiwa.


Uzinduzi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Mtera unatajwa kuwa mkombozi wa uchumi wa maeneo ya kati na nyanda za juu kusini, kwa kuweka mazingira bora ya ukuaji wa viwanda, ujasiriamali na ajira, hivyo kuboresha maisha ya Watanzania na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.







🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post