Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Deus Sangu, amewataka watumishi wa umma, hususan wa serikali za mitaa, kuzingatia maadili ya kazi na utumishi wa umma ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima pamoja na vitendo vya ubadhirifu wa fedha na mali za umma.
Wito huo umetolewa leo Januari 15, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha 31 cha Baraza la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU).
Akizungumza katika kikao hicho, Sengu amesema migogoro inayojitokeza baina ya watumishi wa umma na viongozi wa serikali au wanasiasa mara nyingi husababishwa na kutokuzingatiwa kwa maadili ya kazi, ikiwemo vitendo vya uongo, uzembe na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Ameeleza kuwa mikutano ya vyama vya wafanyakazi ni haki ya kikatiba na kwamba serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na vyama hivyo katika kutatua changamoto na migogoro ya watumishi, ikiwemo kuwatetea pale wanapofanyiwa vitendo vinavyokiuka maadili, kama vile kudhalilishwa kwa lugha isiyo ya staha au kulazimishwa kufanya kazi chini ya mazingira yasiyokidhi viwango.
Sangu amesisitiza kuwa watumishi wa serikali za mitaa ni mhimili muhimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi, akibainisha kuwa Rais wa Awamu ya Sita anaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kupandisha madaraja, kuajiri watumishi wapya hasa katika sekta ya afya na kuimarisha vyama vya wafanyakazi.
Akizungumzia malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo ya fedha za likizo, Sangu amesema mapendekezo yalishawasilishwa serikalini na kubainisha kuwa fedha za malimbikizo ya likizo kwa watumishi wa serikali za mitaa zinapatikana na zitaendelea kulipwa.
Kuhusu miundo ya utumishi, amesema baadhi ya miundo imeanza kurekebishwa baada ya kubainika kuwepo kwa watumishi waliokuwa wakiongeza elimu bila kunufaika katika ajira zao.
Awali, akisoma risala ya TALGWU, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Komredi Wandiba Ngocho, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kushughulikia kero za watumishi wa umma, ikiwemo upandishwaji wa madaraja, ujenzi wa vituo vya afya, utoaji wa mafunzo na uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu.
Hata hivyo, amesema changamoto ya kutolipwa kwa wakati fedha za likizo bado ni kubwa, akibainisha kuwa baadhi ya watumishi wa serikali za mitaa hawajalipwa tangu mwaka 2018. Ameomba serikali kutenga fedha maalum ili kumaliza tatizo hilo linaloendelea kuongezeka kila mwaka.
Ameeleza pia changamoto nyingine zikiwemo ucheleweshaji wa malipo ya fedha za uhamisho, upungufu wa watumishi wa afya pamoja na baadhi ya wanasiasa kuwanyanyasa au kuwazalilisha watumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU Taifa, Tumaini Yamuhoka, amesema chama hicho si cha migomo bali hupendelea majadiliano ya mezani, akisisitiza kuwa kwa kiasi kikubwa masuala mengi yanayowahusu watumishi yanaendelea kushughulikiwa kwa mafanikio kupitia ushirikiano kati ya serikali na vyama vya wafanyakazi.
🚨Full Video Inapatikana Katika Youtube Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.








