PPRA YAHIMIZA VIJANA KUUNDA VIKUNDI, KUNUFAIKA NA ASILIMIA 30 YA ZABUNI ZA SERIKALI

 


Na Carlos Claudio,Dodoma.📍


SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewahimiza vijana nchini kuunda vikundi, kuvisajili na kujenga makampuni ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa kupitia mfumo wa ununuzi wa umma, hususan mfumo wa kielektroniki wa NeST.


Akizungumza leo Jumamosi Januari 17, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na Mfumo wa NeST kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Biashara Dodoma (CBE), Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba, amesema Serikali imetenga asilimia 30 ya fedha za ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.


Simba amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa mapema kuhusu fursa za zabuni za serikali na kuwaandaa kuingia kwenye sekta ya ununuzi wa umma mara baada ya kuhitimu masomo yao.


“Tunataka vijana waache fikra za kusubiri ajira pekee, bali waanze kujipanga kuwa waajiri kwa kuanzisha makampuni yatakayoweza kushiriki kwenye zabuni za serikali. Fursa zipo nyingi na zikitumika vizuri zinaweza kuwajenga kiuchumi hadi kufikia hatua ya kuwa wafanyabiashara wakubwa,” amesema Simba.


Ameongeza kuwa PPRA imejipanga kutembelea vyuo vikuu vyote nchini ili kutoa elimu kuhusu sheria, taratibu na fursa zilizopo katika ununuzi wa umma, hatua itakayosaidia kuongeza ushiriki wa vijana katika mfumo huo na kupanua wigo wa wanufaika wa zabuni za serikali.



Kwa upande wake, Meneja wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Gilbart Kamde, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwafungua macho wanafunzi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya ununuzi wa umma na kuwahamasisha kuiona sekta hiyo kama eneo muhimu la ujasiriamali.


Kamde amesema kupitia elimu hiyo, vijana wataweza kujifunza namna ya kuanzisha biashara, kusajili makampuni, kutumia mfumo wa NeST na kushiriki kikamilifu katika zabuni za serikali kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.


Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wamesema mpango huo umewapa mwanga mpya, hasa katika kipindi ambacho vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira. 


Wamesema elimu waliyopata imewajengea matumaini ya kuanzisha biashara, kukuza makampuni yao na kutumia fursa za zabuni za serikali kama njia ya kujikwamua kiuchumi.



Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwawezesha vijana kiuchumi na kuongeza ushiriki wa makundi maalum katika shughuli za ununuzi wa umma nchini.








🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post