CCM YAONYA KAULI ZA JAZBA, YATANGAZA ZIARA YA KITAIFA KUANZIA SINGIDA

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya vikali dhidi ya kauli na mienendo inayopotosha ukweli, kuchafua historia ya Taifa na kuhujumu amani ya nchi kwa maslahi binafsi, kikisisitiza kuwa hakitaruhusu siasa za jazba, chuki na migawanyiko kuendelea.


Onyo hilo limetolewa leo Januari 17, 2026 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.


Kihongosi amesema CCM ni chama kinachojengwa juu ya misingi ya maridhiano, umoja na kuheshimiana, hivyo hakitovumilia juhudi zozote za kupotosha ukweli au kueneza chuki zisizo na tija kwa maendeleo ya Taifa.


Ameeleza kuwa chama kinamheshimu Waziri Mkuu na Jaji Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa, lakini kikamtaka kuendelea kufurahia maisha ya kustaafu kwa utulivu bila kutoa malalamiko yanayoweza kuleta tafsiri hasi kwa umma.


“Ni jambo la kawaida kwa viongozi waliolitumikia Taifa kuheshimiwa, lakini wastaafu wanapaswa kutoa nafasi kwa viongozi waliopo kuendelea na majukumu yao,” amesema Kihongosi.


Ameongeza kuwa licha ya Jaji Warioba kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, bado alionekana mitandaoni akitoa kauli zenye malalamiko, hali ambayo CCM imeitaja kuwa haina tija kwa maendeleo ya Taifa.


Akizungumzia masuala ya kichama, Kihongosi ametangaza kuwa kuanzia Januari 18, 2026, ataanza ziara ya kitaifa itakayohusisha mikoa yote ya Tanzania, ikianzia mkoani Singida. Ziara hiyo inalenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kuimarisha chama pamoja na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za Rais Samia.


“Ziara hii ni jukwaa la wananchi. Kama kuna anayehisi kuonewa au kunyanyaswa, tunawakaribisha waje ili tusikilize na kutatua changamoto zao,” amesema.


Katika hatua nyingine, Kihongosi amempongeza Rais Samia kwa kukutana na Mabalozi wa Tanzania Januari 15, 2026 katika kikao cha ufunguzi wa mwaka, akisema mkutano huo umeimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa na kuonesha mwelekeo chanya wa diplomasia ya nchi.


Pia ametoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi, ambapo makusanyo yamefikia shilingi trilioni 3.1, huku mwezi Desemba yakivuka zaidi ya shilingi trilioni nne.


Kuhusu masuala ya kijamii, Kihongosi amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa bima ya afya kwa wote, sambamba na kuchukua hatua za kuondoa tabia ya kuzuia maiti za wagonjwa wasiolipa gharama za matibabu.


Aidha, ameeleza kuwa Serikali imetekeleza ahadi yake ya ajira kwa kutoa ajira zaidi ya 12,000 katika sekta mbalimbali, huku mpango wa kutoa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuwawezesha vijana ukiendelea kutekelezwa nchini.



🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post