Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imesisitiza umuhimu wa Serikali kuweka mifumo madhubuti ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi kupata mitaji na zana za kazi, ikibainisha kuwa vijana wengi hushindwa kuendeleza ujuzi walioupata baada ya kuhitimu kutokana na ukosefu wa rasilimali hizo muhimu.
Akizungumza Januari 24, 2026 wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati hiyo Wilayani Chemba mkoani Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mkoa wa Tanga, Husna Jumbe, amesema upatikanaji wa mitaji kwa wahitimu wa vyuo vya VETA utawawezesha vijana kuwa sehemu ya majibu ya changamoto za kijamii kwa vitendo badala ya kubaki na vyeti pekee.
Amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya elimu ya ufundi stadi lazima uendane na ubora wa mafunzo yanayotolewa, akisisitiza kuwa majengo, vifaa, mifumo ya TEHAMA na mitaala ya kisasa vinapaswa kuambatana na uwepo wa walimu wenye weledi na mafunzo yanayokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Bila kuzingatia ubora, uwekezaji wa fedha pekee hautaleta matokeo yaliyokusudiwa. VETA inapaswa kuhakikisha kila rasilimali inayowekezwa inazalisha wahitimu wenye ujuzi unaoweza kutatua changamoto za kijamii na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa,” amesema Jumbe.
Ameongeza kuwa vyuo vya VETA vimepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hususan katika upanuzi wa miundombinu, ongezeko la kozi, ubora wa mafunzo na usambazaji wa vyuo hadi ngazi ya wilaya, hali iliyofanya elimu ya ufundi stadi kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya rasilimali watu nchini.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo, Asha Baraka, amesema VETA inapaswa kubuni mafunzo yanayojibu moja kwa moja changamoto za kijamii ili kuvutia vijana zaidi kujiunga na vyuo vya ufundi stadi.
Amesema mafunzo hayo yanapaswa kulenga maeneo muhimu kama upatikanaji wa maji safi, nishati ya umeme, makazi bora na huduma nyingine za msingi.
Asha ameongeza kuwa kuna haja ya VETA kuwekeza zaidi katika mafunzo ya ufundi wa viatu yanayokidhi mahitaji ya Watanzania wa makundi yote, akisema mafunzo hayo yakizingatia mazingira ya ndani, kipato cha wananchi na ubora wa bidhaa, yatawasaidia vijana kuzalisha viatu vinavyoshindana sokoni na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Bakar Shingo, ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu ya maji katika Chuo cha VETA Chemba pamoja na ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama wa wanafunzi na mali za chuo.
Pia amependekeza kuanzishwa kwa kozi zinazozingatia mazingira ya Wilaya ya Chemba ili kuwasaidia vijana kujiajiri na kuchangia maendeleo ya eneo lao.
Naye Mabula Magangila amesema kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya soko la ajira, VETA inapaswa kuendelea kubuni miradi bunifu inayochanganya ufundi wa jadi na teknolojia ya kisasa, ikiwemo utengenezaji wa mashine ndogo, nishati mbadala na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthon Kasore, amesema VETA imejikita katika kuimarisha upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi kwa usawa, kuboresha ubora wa mafunzo na kuendeleza ubunifu unaoendana na vipaumbele vya taifa.
Amesema kati ya mwaka 2021 hadi 2026, jumla ya wanafunzi 430,416 wamedahiliwa katika vyuo vya VETA nchini, wakiwemo 1,830 wenye mahitaji maalum na 6,515 wanaotoka katika mazingira magumu.
Aidha, kupitia Mpango wa Ukuzaji Ujasiriamali katika Sekta Isiyo Rasmi (INTEP), wajasiriamali 6,501 wamepatiwa mafunzo ya kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omar, amesema Wizara inaendelea kutafakari mbinu bora za kuwawezesha wahitimu wa VETA kupata mitaji kupitia vikundi ili kuongeza uwajibikaji na usimamizi wa fedha.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Wanu Ameir, amesema Serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ufundi stadi kwa kuboresha mazingira ya mafunzo, kuhuisha mitaala na kuhakikisha vijana wanapata nyenzo zitakazowawezesha kubadili ujuzi wao kuwa fursa za kiuchumi.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.











