Dodoma.📍
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Tanzania Sports Influencers limefanya mazoezi ya pamoja yaliyoambatana na michezo mbalimbali ikiwemo jogging na mpira wa miguu, kwa lengo la kuhamasisha amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Mazoezi hayo yamefanyika Januari 24, 2025, yakihusisha wananchi wa kada mbalimbali pamoja na vikundi vya jogging kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Dodoma. Shughuli hiyo imeongozwa na Afisa na Mnadhimu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) William Mwamamfupa.
Akizungumza katika tukio hilo, ACP Mwamamfupa amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani na kuimarisha umoja, pamoja na kutoa taarifa za wahalifu au watu wenye nia ovu ili kudhibiti na kuzuia vitendo vya kihalifu.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wananchi wake unaimarishwa kwa kuzuia uhalifu na kutoa elimu ya usalama kwa makundi mbalimbali ya kijamii kupitia bonanza za michezo na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
Kwa upande mwingine, ACP Mwamamfupa amepongeza Tanzania Sports Influencers kwa ushirikiano wao na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, akisema ziara yao mkoani humo inalenga kuunga mkono timu za Taifa pamoja na kukuza na kuibua vipaji vya michezo, hususan kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) inayotarajiwa kufanyika hapa nchini.
Amesisitiza kuwa michezo ni chombo muhimu katika kujenga afya, umoja na amani, hivyo kuendelea kuhimiza ushiriki wa wadau mbalimbali katika shughuli za kijamii zitakazochangia maendeleo ya taifa.





