VETA NI SULUHU YA CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA – MAGANYA


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya, amesema mafunzo yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni suluhu muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini.


Maganya ameyasema hayo Januari 17, 2026, wakati wa ziara ya viongozi wa Umoja wa Wazazi wa Tanzania katika Makao Makuu ya VETA jijini Dodoma, akibainisha kuwa kupitia VETA taifa linaelekea kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.


Amesema wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwaelekeza vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi na kuwajengea misingi ya kujiajiri, ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi.


Aidha, Maganya ametoa wito kwa jamii kuondoa mtazamo hasi dhidi ya mafunzo ya ufundi yanayotolewa na VETA, akisisitiza kuwa mafunzo hayo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa na chanzo kikubwa cha ajira. 


Ameongeza kuwa kozi mbalimbali za VETA zinawawezesha vijana kujiajiri, huku akibainisha kuwa changamoto ya ajira ni ya kidunia na Tanzania ipo katika hali ya kawaida ikilinganishwa na nchi nyingine.


Ameeleza kuwa kwa sasa wahitimu wenye ujuzi wa VETA wanapewa kipaumbele katika soko la ajira, na kwamba Chama cha Mapinduzi kinatambua na kuunga mkono jitihada za serikali yake katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana kupitia mafunzo ya ufundi.



Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omar, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Prof. Adolf Mkenda, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana dhamira ya dhati ya kuona vijana wa Kitanzania wanapata ajira.


Dkt. Omar amesema kuwa kupitia serikali ya CCM, sera ya elimu ilifanyiwa maboresho kwa kuweka mkazo zaidi kwenye elimu ya ujuzi, hatua inayolenga kuwawezesha vijana kuajirika au kujiajiri.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa VETA imeongeza vyuo zaidi ya 30 katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini, na hivyo kufikia jumla ya vyuo 80. Ameongeza kuwa vyuo 65 vinaendelea kujengwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuondoa changamoto ya vijana kukosa ujuzi na ajira.


Kasore amesema udahili umeongezeka kutoka wanafunzi 61,000 hadi 86,000 kwa mwaka kwa kozi za muda mfupi na muda mrefu, huku serikali ikigharamia ada za masomo kwa asilimia kubwa ya wanafunzi wa VETA.


Amefafanua kuwa serikali imetumia takribani shilingi bilioni 7.2 kununua vifaa vya kisasa vya kujifunzia kwa vyuo vya zamani ili viendane na mabadiliko ya teknolojia, ambapo zaidi ya vyuo 60 vimepatiwa vifaa hivyo.


Aidha, amesema muitikio wa watoto wa kike kujiunga na mafunzo ya ufundi umeongezeka kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30, jambo linaloonesha mabadiliko chanya katika jamii.



Kasore pia amesema VETA kwa sasa inatoa mafunzo ya kurasimisha ujuzi kwa watu ambao hawakupitia elimu rasmi lakini wana ujuzi walioupata katika mazingira ya kazi, ambapo zaidi ya vijana 22,000 tayari wamesharasimisha ujuzi wao na kupata vyeti. Ameongeza kuwa mpango ni kuwafikia vijana 100,000 kote nchini ili kuhakikisha kila mkoa unanufaika na mpango huo.









🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post