Na Mwandishi Wetu.
Kampuni ya Xmation Digital imezindua rasmi ofisi yake mpya na kutangaza mpango mahsusi wa kuwawezesha vijana kujifunza masuala ya teknolojia na ubunifu wa kidijitali, ikiwa ni hatua muhimu katika kukuza ujuzi wa sekta hiyo nchini.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi wa kampuni, waandishi wa habari, wadau wa teknolojia na wageni mbalimbali, ambao kwa pamoja walipongeza juhudi za kampuni hiyo katika kuchochea maendeleo ya kidijitali.
Akizungumza katika hafla hiyo, uongozi wa Xmation Digital ulieleza kuwa uzinduzi huo ni ishara ya dhamira yao ya kuijenga jamii inayotumia teknolojia kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi. Viongozi hao walisisitiza kuwa ofisi mpya itakuwa kitovu cha ubunifu, mafunzo na huduma za kisasa zitakazowasaidia vijana na wataalamu kukuza vipaji vyao.
Viongozi wa kampuni hiyo walitoa shukrani kwa wadau wote waliochangia mafanikio ya hatua hiyo muhimu, wakisema kwamba ushirikiano kutoka kwa washirika, familia, marafiki na jamii kwa ujumla umekuwa msingi wa safari yao ya mafanikio. Aidha, waliwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kuifikisha taarifa sahihi kwa jamii.
Xmation Digital imeahidi kuendelea kushirikiana na vijana, taasisi na jamii kwa ujumla katika kujenga mustakabali bora wa teknolojia, ubunifu na uchapishaji nchini, sambamba na kuwa chachu ya mabadiliko katika dunia ya kidijitali.






